2015-11-21 10:24:00

Baba Mtakatifu Francisko karibu sana katika Nchi za AMECEA!


Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA kwa niaba ya Familia ya Mungu kutoka katika nchi zote zinazounda AMECEA anapenda kuchukua nafasi hii kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi za AMECEA kwa kutembelea: Kenya na Uganda. Anasema, Bara la Afrika lina umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Yesu kwani Barani Afrika, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ili pata hifadhi wakati maisha ya Mtoto Yesu yalipokuwa hatarini. Yesu akapata maskani ya muda nchini Misri na mambo yalipokuwa shwari wakarejea tena katika Nchi Takatifu.

Kardinali Souraphiel anakaza kusema, AMECEA inajiona kuwa imepata upendeleo wa hali ya juu,  kwa kutembelea Kenya mahali ambako AMECEA ina makao yake makuu. Hili ni Shirikisho linayoyaunganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi kumi na moja, lakini pia kuna Mabaraza ya Maaskofu kutoka Djibouti na Somalia ambayo yanashirikishwa na AMECEA. Familia ya Mungu katika nchi hizi imekuwa ikisali kwa ajili ya kufanikisha hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika anapokuja kuwaimarisha ndugu zake katika imani.

Kardinali Souraphiel anaonesha msisitizo wa pekee kwa kusema kwamba, Familia ya Mungu Barani Afrika katika ujumla wake inapenda na kuthamini Injili ya uhai na inataka kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai hadi kieleweke! Bara la afrika linawaheshimu sana wazee na wageni na wako mstari wa mbele katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. AMECEA inapenda kukuza na kudumisha tunu hizi msingi katika maisha na utume wa Kanisa dhidi ya mila na tamaduni ambazo zimepitwa na wakati.

Familia ya Mungu inatambua kwamba, watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanapaswa kupendwa, kuheshimiwa na kulindwa dhidi ya nyanyaso na dhuluma wanazoweza kukumbana nazo kwa kufanyishwa kazi za suluba; kupelekwa mstari wa mbele kama chambo katika vita; kunyanyaswa kijinsia au kutumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na viungo kwa njia ya uhamiaji haramu. Familia ya Mungu kutoka katika Nchi za AMECEA inapenda kwa moyo mkuu na wa shukrani kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuwapa neno na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu Francisko karibu sana AMECEA!

Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa mtandao wa AMECEA. 








All the contents on this site are copyrighted ©.