2015-11-20 08:12:00

Utamaduni wa afya, ukarimu na utunzaji bora wa mazingira ni muhimu sana!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anasema, maadhimisho ya mkutano wa thelathini wa afya kimataifa unalenga kuibua mbinu mkakati ya kumhudumia mwanadamu vyema zaidi sanjari utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa utunzaji bora wa mazingira. Mkutano huu umefunguliwa rasmi hapo tarehe 19 Novemba kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani na baadaye wajumbe wakakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Askofu mkuu Zimowski anasema, mkutano huu unafanyika wakati ambapo Mama Kanisa anajiandaa kwa namna ya pekee kabisa kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu hapo tarehe 8 Desemba 2015. Mkutano huu unaongozwa na kauli mbiu “Utamaduni wa afya na ukarimu kwa ajili ya huduma kwa binadamu na dunia katika ujumla wake”. Huu ni mkutano unaojaribu kupembua uhusiano uliopo kati ya afya binadamu na uharibifu wa mazingira kadiri ya Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si!

Askofu mkuu Zimowski anakaza kusema, waamini waalikwa kwa namna ya pekee kuwa kweli ni vyombo vya huduma kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha Yesu Kristo Msamaria mwema, aliyejinyenyekesha, akajishusha ili kumganga mwanadamu kiroho na kimwili. Huduma ya afya inayotolewa kwa binadamu inapaswa kujikita katika utu wa binadamu, upendo na heshima ya binadamu. Hii ni changamoto na dhamana ambayo waamini kwa namna ya pekee wamejitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo.

Askofu mkuu Zimowski anaendelea kufafanua kwamba, katika maadhimisho ya mkutano huu wa thelathini wa afya kimataifa; Injili ya uhai, utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pamoja na utunzaji bora wa mazingira ili kuepusha magonjwa yanayotokana na uharibifu wa mazingira ni kati ya mambo yanayopewa msukumo wa pekee kwa sasa.

Mkutano huu pamoja na mambo mengine unapania kuwa ni chachu ya maboresho katika maisha ya watu wengi, kwa kujikita katika huduma ya afya yenye mwelekeo chanya, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza sanjari na utunzaji bora nyumba ya wote. Ni changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu na badala yake kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, maskini na wazee.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anauweka mkutano wa thelathini wa afya kimataifa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu; ili waweze kuwasaidia wajumbe wa mkutano huu kuuangalia ulimwengu kwa jicho la hekima; Mtakatifu Yosefu msimamizi wa Familia Takatifu aendelee kulisimamia na kulilinda Kanisa bila binadamu kusahau dhamana ya utunzaji bora wa mazingira, kazi waliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu; pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa familia ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.