2015-11-20 10:54:00

Msumbiji inaishukuru Serikali ya Angola kwa kuifutia deni kwa asilimia 50%


Serikali ya Angola imeamua kufuta asilimia 50% ya deni la njekwa serikali ya Msumbiji linalokadiriwa kuwa ni zaidi ya dolla za kimarekani millioni 600 kama kielelezo cha urafiki na mshikamano kati ya mataifa haya mawili. Tamko hili limetolewa na Serikali ya Angola mara baada ya Rais Filipe Nyusi kuhitimisha safari ya kikazi nchini Angola kwa lengo la kuendelea kuimarisha mahusiano mema kati ya nchi hizi mbili.

Wakati huo huo, habari kutoka Maputo, Msumbiji zinabainisha kwamba, hali ya kisiasa si shwari sana nchini Msumbiji baada ya Serikali kuamua “kula sahani moja” na wanajeshi wa RENAMO hadi kieleweke. Hivi karibuni kumezuka mapigano makali kati ya Jeshi la Serikali pamoja na wanajeshi wa RENAMO, ili kuwanyang’anya silaha ambazo zimekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa misingi ya amani na utulivu. Kutokana na mapambano haya, Bwana Alfonso Dhlakama hajulikani aliko kwa kuhofia usalama wa maisha yake.

Mapambano haya yamefanyika kwenye ngome ya RENAMO huko Beira, Sofala. Kunako mwaka 1992 RENAMO na FRELIMO walitiliana sahihi mkataba wa amani na kati ya masharti yalikuwa ni kuwajumuisha wanajeshi wa RENAMO katika jeshi la umoja wa kitaifa pamoja na wanajeshi hawa kusalimisha silaha zao kwa Serikali. Vita na vurugu za kisiasa zimekuwa zikirudisha nyuma jitihada za Msumbiji kujikwamua kutoka katika historia yake iliyopita kwa kuendelea kuendekeza vita ya wenyewe kwa wenyewe badala ya kujikita katika majadiliano, umoja wa kitaifa na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.