2015-11-20 09:20:00

Kanisa lina matumaini makubwa katika Injili ya familia!


Askofu James Maria Wainaina Kungu wa Jimbo Katoliki Murang’a, Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia yaliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican yaliyongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo”. Hii ilikuwa ni nafasi kwa Mababa wa Sinodi kutafakari, kusali na hatimaye kutoa mapendekezo kuhusu maisha na utume wa familia kwa Baba Mtakatifu Francisko, tayari kuyafanyia kazi kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayokumbana na changamoto nyingi sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu Wainaina anakaza kusema, maadhimisho ya Sinodi ya familia yalijikita katika hati ya kutendea kazi ya Sinodi ya Maaskofu ambayo ni matunda ya hati elekezi iliyotolewa na Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya familia iliyofanyika kunako mwezi Oktoba 2014. Lengo ni kuzijengea familia uwezo wa kutangaza, kushuhudia na kutetea Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai na matumaini kwa binadamu.

Baada ya tafakari ya kina, hatimaye, Mababa wa Sinodi waliwasilisha mapendekezo yao kwa Baba Mtakatifu Francisko tayari kuyafanyia kazi. Ni matumaini ya Askofu James Wainaina Kungu kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ataweza kutoa dira na mwongo wa Injili ya familia kwa watu wa nyakati hizi. Katika maadhimisho ya Sinodi ya Familia, Mababa wamechambua kwa kina kuhusu familia mintarafu hali za kibinadamu, kijamii na kitamaduni; familia na changamoto za kijamii na kiuchumi; mwingiliano wa familia na jamii husika; familia mintarafu Mpango wa Mungu: familia katika historia ya wokovu; familia katika mafundisho ya Mababa wa Kanisa; familia kadiri ya mafundisho ya Kikristo; utimilifu wa uelewa wa familia kadiri ya Kanisa.

Askofu Wainaina anaendelea kusema kwamba, Mababa wa Sinodi waligusia kwa kina na mapana kuhusu utume wa familia kwa kukazia majiundo endelevu ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; malezi pamoja na kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na kwamba, Kanisa linapaswa kuibua mbinu mkakati makini kwa ajili ya utume wa familia, ili kuziwezesha familia kuwa ni vyombo vya Unjilishaji mpya.

Kuna familia nyingi duniani zinazokumbana na hali ngumu ya maisha kutokana na umaskini, magonjwa, dhuluma na nyanyaso. Kuna baadhi ya watu wanalazimika kuzikimbia nchi na familia zao; magonjwa pamoja na kuporomoka kwa tunu bora za maisha ya ndoa na familia. Yote haya ni matatizo na changamoto zinazoendelea kuzikabili familia nyingi! Kutokana na matatizo na changamoto zote hizi, familia za Kikristo zinapaswa kuwa kweli ni imara na thabiti katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbata uhai na matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.