2015-11-20 07:23:00

Jengeni utamaduni wa udugu na umoja ili kutetea maisha na kutunza mazingira


Umoja na udugu ni mambo msingi yanayoweza kuwakutanisha watu kutoka katika lugha, jamaa na dini mbali mbali pasi na ubaguzi, ikiwa kama Jamii itajikita katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa afya na ukarimu kwa ajili ya huduma kwa binadamu na dunia katika ujumla wake. Ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 19 Novemba 2015 alipokutana na kuzungumza na wajumbe zaidi ya 550 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaohudhuria mkutano wa thelathini wa kimataifa ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Mkutano huu umeanza hapo tarehe 19 Novemba na utafungwa rasmi hapo tarehe 21 Novemba 2015.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ulimwengu mamboleo unaendelea kujikita katika ubaguzi kwa baadhi ya watu wasiokidhi vigezo vya dawa ya tamaa inayotaka ukamilifu kwa gharama yoyote ile, hata kama utu na heshima ya binadamu vitawekwa rehani. Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa Injili ya Maisha, “Evangelium vitae”, waraka muhimu sana katika kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu pamoja na kujikita katika ukarimu, huruma, uelewa na msamaha; mambo msingi katika huduma kwa wagonjwa wa kiroho na kimwili.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Yesu Kristo ni mfano na kielelezo cha ujirani mwema kwa wagonjwa, wadhambi, waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu, maskini, wageni na wote waliokuwa wanatengwa na jamii kwa wakati ule!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata leo hii makundi haya ya watu bado yamo katika jamii na kwamba yanaendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii kana kwamba watu hawa si mali kitu! Hiki ni kielelezo cha utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, kinyume kabisa cha utamaduni unaofundishwa na Yesu, utamaduni unaojikita katika upendo na mshikamano kwa kujali na kuthamini maisha na utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hiki ni kielelezo cha ujenzi wa umoja na udugu unaovuka mipaka ya matabaka ya kijamii, kiitikadi na imani ya mtu. Waamini wanaalikwa kuwa kweli ni Wasamaria wema kwa jirani zao.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, ujirani mwema unavuka hata ule utamaduni wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kama unavyojionesha kwa mataifa tajiri hata wakati mwingine kwa mataifa maskini duniani; au maskini wanaojihesabu kuwa ni watu kwa kutumia vigezo vya umuhimu wao na uzalishaji katika masuala ya kiuchumi. Hii ni dhana ambayo inajikita katika dawa ya kufikirika kwa kuwa na matamanio ya kufikia utimilifu kwa gharama yoyote ile ya maisha. Kuna mchakato wa tafiti unaoendelea kufanyika kwenye Nchi tajiri zaidi duniani kwa kutafuta ukamilifu wa kimwili pamoja na ujana usiokuwa na kikomo; mambo ambayo yanawatenga watu wasioweza kukidhi vigezo hivi kwani wanahesabiwa kuwa ni mzigo, usumbufu na watu wasiofaa katika jamii.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna uhusiano wa karibu kati ya afya na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni changamoto ya kujikita katika uwajibikaji, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kuwajali na kuwathamini maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ukosefu wa utunzaji bora wa mazingira ni chanzo kikuu cha magonjwa katika jamii.

Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano wa thelathini wa afya kimataifa kwa kuwatia shime kuwa makini katika huduma kwa kuzingatia uhalisia wa maisha ya watu wanaowahudumia katika maeneo yao; watu ambao wengi wao ni wahanga wa athari za mabadiliko ya tabianchi; mambo ambayo yanachangia kudhohofisha afya ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.