2015-11-18 07:56:00

Kanisa Katoliki Tanzania linaendelea kufanya maboresho makubwa katika elimu


Askofu John Ndimbo kutoka Sektretarieti ya huduma za kijamii Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha baadhi ya changamoto zinazoikumba sekta ya elimu nchini Tanzania na jinsi ambavyo Kanisa linajitahidi kuboresha sekta hii katika taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuanzia shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu.

Idara ya elimu kitengo cha huduma za kijamii cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kimeamua kuunda kitengo cha ukaguzi kitakachofanya tathmini kuhusu: kiwango na ubora wa elimu inayotolewa kwa watanzania na Kanisa Katoliki, tayari kutoa ushauri kwa wadau mbali mbali ili kurekebisha au kuboresha zaidi pale inapoonekana kwamba, inafaa.

Idara ya elimu kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Mtakatifu Augostino cha Tanzania, SAUT kimekuwa kikiendesha semina za mara kwa mara kwa wakuu wa shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyoendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania, ili kuwapatia sera na mikakati ya stadi za uendeshaji wa taasisi za elimu zinazomilikiwa na Kanisa Katoliki Tanzania. Kanisa linatambua kwamba, hii ni huduma muhimu sana katika jamii inayopaswa kutolewa pasi na ubaguzi wa imani au itikadi ya mtu. Kanisa linashirikiana kwa karibu sana na Serikali katika mchakato wa maboresho ya elimu kadiri ya miongozo, taratibu na kanuni zinazotolewa na Serikali chini ya mwamvuli wa wadau wa sekta binafsi ya elimu nchini Tanzania.

Majimbo mbali mbali yanaendelea kuboresha miundo ya sekta ya elimu ili kukidhi ubora na viwango vinavyotolewa na Idara ya elimu anasema Askofu Ndimbo. Jambo linalotia moyo na faraja kuu ni kuona jinsi ambavyo Maaskofu wanaendelea kuwekeza katika majiundo makini ya rasilimali watu kwa kuwasomesha Wakleri na Watawa tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uongozi kwa taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Tanzania. Cheche za mafanikio haya zinaanza kujionesha nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.