2015-11-18 10:23:00

Hali ya hewa imechafuka Ikulu, huko ni patashika nguo kuchanika!


Binadamu ana huluka ya kutaka ukuu, heshima na utukufu! Katika historia ya ulimwengu kumetokea mapigano kati ya watawala wa mataifa makubwa kama vile mafarao wa Misri, wafalme wa Assiria, wa Persia, wa Babiloni, Wagiriki na Warumi wakiwania kupanua himaya zao na kutawala ulimwengu. Kadhalika katika Afrika machifu, manduna, mankosi na watemi wa makabila mbalimbali walipigana vita vikali ili kupanua maeneo ya tawala zao.

Mwishoni mwa karne ya kumi na tisa, mataifa ya Ulaya yakaigawa duniani kama keki katika makoloni ya kutawala. Katika robo ya kwanza ya karne ya ishirini wakaibuka mafashisti, kila mmoja akiwania kuuweka ulimwengu mzima chini ya miguu yake. Ushindani huo ukapelekea kulipuka vita vya kwanza na vya pili vya dunia. Katika mazingira haya ya ushindani wa kumiliki dunia mwaka 1925 Papa Pius X akaitangaza sikukuu ya “Yesu Kristo Mfalme,” kuwa Yesu Kristo ndiye Mtawala pekee wa ulimwengu na ufalme wake unajikita katika ukweli na uzima; utakatifu na neema; haki, mapendo na amani ya kweli ambayo inabubujika kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu!

Mapambano ya ukuu bado yanaendelea hadi leo. Ulimwengu umejaa pilikapilika za mivutano na ushindani wa kutafuta ukuu na kutawala katika nyanja za uchumi yaani katika biashara. Mataifa tajiri yanawania kumiliki rasilmali za mataifa fukara, kama vile ardhi, mafuta, dhahabu, almasi, mito,  maziwa na misitu. Kuna ushindani wa ukuu hata ndani ya dini na madhehebu ya dini, kila mtu anataka apewe sifa na utukufu!

Leo tutashuhudia mahojiano makali kati ya vigogo wawili yahusuyo mtawala mwenye hati miliki ya ulimwengu huu na vigezo vyake. Malumbano hayo yatafanyika Ikulu sehemu maalumu iitwayo Praitorio. Lugha ya mahojiano ni Kigiriki – lugha ya kiofisi ya wakati huo ambayo vigogo wote wawili walitegemewa wajue kuimung’unya, kwani mmoja alikuwa Mrumi mwenye lugha mama Kilatini na mwingine Mwebrania, mwenye lugha mama Kiaramayo.

Kigogo wa kwanza ni Pilato, mwakilishi wa utawala wa Kirumi uliokuwa unashikilia hati miliki ya Uyahudi na ulimwengu mzima. Kigogo wa pili ni Yesu Kristo, ambaye alipoanza kazi Galilea alijitangazia waziwazi kuwa: “Wakati umetimia, na ufame – Utawala –  wa Mungu umekaribia.” (Marko 1:14). Katika Injili tamko hilo linanukuliwa mara mia moja na nne. Kwa hiyo Yesu  ndiye mmiliki halisi aliyejenga ulimwengu huu lakini hati yake miliki imeporwa na wababaishaji. Mazingira ya awali ya mahojiano hayo yalikuwa hivi: Yesu alikuwa ameshikwa na wakuu wa Makuhani na Mafarisayo wakimtuhumu kwa kutenda mabaya. Hivi wakampeleka kwanza kwa Kuhani mkuu Ana, halafu wakampitisha kwa Kayafa. Hatua ya pili wanampeleka kwa Pilato mwakilishi wa Serikali ya Kirumi. Sasa endelea: “Wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, kwa Pilato, lakini wao wenyewe hawakuingia ndani ya ile Praitorio wasije wakanajisika, bali wapate kuila Pasaka.” (Yoh. 18:28).

Praitorio ni moja ya sehemu saba maalumu za Protokali ya Ikulu. Sehemu hizo unazisikia wakati huu wa mashtaka ya Yesu jinsi anavyozungushwa toka sehemu moja hadi nyingine. Kwa vile Praitorio ilikuwa sehemu aliyokuwa anakaa Pilato, huko Makuhani na Mafarisayo walibaki mlangoni hawakuingia ndani wasije wakajinajisi kwa Mrumi mpagani na kafiri, kwa vile jioni ile ilibidi waende Hekaluni kwenye ibada za ufunguzi wa maadhimisho ya Pasaka yao (Yoh 18:28). Pilato akajitokeza hapo mlangoni na kuwauliza: “Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?” Baada ya kurushiana maneno mawili matatu na Makuhani, Pilato akaingia ndani ya Praitorio na kumwita Yesu. Hebu sasa fuatilia kwa makini kilichojiri mle ndani, ambamo wakuu hawa wawili waliwekana kiti moto. Malumbano hayo yatakusaidia kupembua na kupembua zaidi juu ya utawala na ukuu ulio bora na siyo bora ukuu, tunaotakiwa kuuwania katika maisha.

Pilato akampachika Yesu swali la kwanza: “Wewe ni mfalme wa Wayahudi?” Yoh. 30:46. Swali hilo ni kinyume kabisa na mashtaka waliyomtuhumu. Wayahudi walisema: “Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako” (Yoh 18: 30). Kwa hiyo swali la Pilato liko nje ya mada. Yesu anapoona swali la Pilato linakosa mantiki, akamgeuzia kibao bila woga wala kunyanzi na kumtaka ajieleze zaidi: “Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?” (Yoh. 18:34) maana yake, kama Pilato ametonywa na Wayahudi kwamba Yesu anajidai kuwa Mfalme wa Wayahudi, hapo yamaanisha ni Mfalme yule aliyetabiriwa na Manabii yaani, Masiha atakayewakomboa. Kama ndivyo, basi hicho ni kigezo cha mfalme aliye mpakwa yaani Kristo. Lakini kama Pilato anasema kwa nafsi yake tu, hapo tafsiri ya Mfalme ni ile ya utawala wa Kirumi yaani, kadiri ya vigezo vya ulimwengu huu.

Swali hilo la Yesu lilimchefua na kutibua nyongo ya Pilato hata akamtupia lugha ya kebehi: “Ama! Ni Myahudi mimi!” Lugha hii inadhihirisha kuwa Pilato alimaanisha ufalme wa Kiyahudi, ndiyo maana akaendelea kuhoji: “Taifa lako na wakuu wa makuhani ndiyo waliokuleta kwangu. Umefanya nini?” (Yoh. 18:) Hapa tena unaona wazi kwamba Wakuu wa Makuhani na Wayahudi ndiyo waliomlia Yesu njama za kumwua kwa vile ameingilia nyanja zao za ukuu na kuteka ngome ya ukuu wao! Hapa hapatoshi mtu wangu, ni patashika nguo kuchanika!

Baada ya kuzigundua fikra za Pilato na Wayahudi juu uzuzu wao wa kutoelewa maana ya ufalme, Yesu anatoa jibu litakalomaliza malumbano na litakalotudhihirishia msimamo wa Pilato akasema: “Ufalme wangu siyo wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi.” Kisha akarudia tena “Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” Kwa maelezo haya, Pilato angeweza kuelewa kuwa mamlaka ya Yesu ni ya ulimwengu ujao. Tafsiri hiyo ni potovu, kwani kiunganishi cha sentensi hiyo yabidi kisomeke hivi: “Ufalme wangu si wa kutoka ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungetokana na ulimwengu huu, wale walionipigia kura, mashabiki na wakereketwa wangenipigania. Lakini ufalme wangu hautokani na hapa.” 

Hapa Yesu anataka kusema kwamba, Mamlaka yahe hayatokani na vigezo vya ulimwengu huu, ingekuwa hivyo, basi pale alipojaribiwa Jangwani angeweza kuafikiana na mshawishi kujenga ufalme kadiri ya vigezo vya ulimwengu huu. Kadhalika, angemwacha Petro kuendeleza mapambano pale alipochomoa upanga na kumkata mtumishi mmoja sikio ili kuutetea utawala wake. Kumbe asili ya mamlaka yote ni Mungu naye Yesu amefika kuudhihirisha ufalme huo hapa ulimwenguni. Ndiyo maana anapoulizwa tena: “Wewe u mfalme basi?” Anajibu: “Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni.”

Kwa maelezo hayo, Pilato bado somo halikumwingia kwani alikuwa hamwelewi huyu Yesu ni Mfalme wa mtindo gani anayeshindwa kujitetea mwenyewe. Lakini anamwona Yesu amefungwa mikono na amepigwa, amesimama peke yake bila mlinzi wala mtetezi na anaongea kwa uhuru wote. Wakati yeye Pilato yuko Ikulu amezungukwa na walinzi na jeshi. Ndipo Yesu anamtolea uvivu anapomweleza kuwa ufalme wake Yesu ni wa kutetea ukweli: “Nimekuja ulimwengu ili kuushuhudia ukweli” (Yoh. 18:37), yaani Yesu amekuja kumshuhudia Mungu halisi Mungu wa kweli, Mungu anayetumikia siyo mtawala wa mabavu. Kwa hiyo, Yesu amejifanya binadamu ili aoneshe jinsi binadamu wa kweli mwenye utu anavyotakiwa kuwa, na siyo binadamu aliyegeuka kuwa mnyama kwa matendo yake. Hata hivyo neno hilo ukweli halikuweza kuingia kichwani mwa Pilato. Anashindwa kuelewa anachomaanisha Yesu juu ya Mtawala wa Kweli, kwa sababu kwake yeye utawala wa kweli ni wa Kirumi yaani ule wa Kaisari Tiberius. Pilato alishatosheka na ukweli wa utawala huo. Mapato yake anauliza swali la dharau huku anaondoka bila kusubiri jibu: “Ukweli ni nini?” (Yoh 18: 38), kama vile angesema. “Utaniambia nini wewe, Unajua ukweli wewe, Hebu ondoka zako!”

Tamko hili la mwisho la Pilato, “Ukweli ni nini!” na kuondoka bila kusubiri jibu, ni onyo na fundisho kubwa sana kwetu tulioyafuatilia malumbano haya. Tunafundishwa kutokung’ang’ana na kile tunachodhani ni ukweli, au tunachofikiri kuwa ni uhalisia wa ukuu, wa madaraka, wa utawala na kutotaka kabisa kusikia wala kuelewa utawala wa haki na upendo wa kweli wa Mungu. Tumfuate Mfalme wa ulimwengu, Yesu aliye Njia Ukweli na Uzima. Heri kwa Sikukuu ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.