2015-11-17 08:48:00

Elimu makini ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga!


Askofu mkuu Angelo Vincenzo Zani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki anasema imekwisha yoyoma miaka hamsini tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu Elimu Katoliki, “Gravissimum educationis”, tamko ambalo hadi leo hii ni endelevu kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa kukabiliana na changamoto za elimu. Ni tamko ambalo limeliwezesha Kanisa kukutana na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, kusikiliza na kuwashirikisha wadau wengine sera na mikakati ya elimu katoliki kwa ajili ya kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili mintarafu mwanga wa haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko ametambua mchango wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ndiyo maana ameridhia kuanzishwa kwa Mfuko wa Elimu utakaosaidia kufanya tafiti pamoja na kuwahudumia watoto wa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili waweze kupata elimu ambayo itawasaidia kuharakisha maboresho ya maisha yao. Kwa kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya binadamu, Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kuanzia tarehe 18 hadi tarehe 21 Novemba 2015, linaendelesha kongamano la kimataifa la elimu katoliki litakalowajumuisha wajumbe kutoka nchi mbali mbali duniani, ili kupanga mwongozo wa jumla na sera za mikakati ya elimu bora inayopaswa kutolewa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Zani anakaza kusema, Mfuko wa Elimu uliaonzishwa hivi karibuni unaonesha msukumo wa pekee kabisa unaotolewa na Kanisa Katoliki katika huduma kwa binadamu kwa kutambua kwamba, elimu ni kikolezo kikuu cha mageuzi na maendeleo ya binadamu kiroho na kimwili. Sekta ya elimu ni sehemu muhimu sana ya Uinjilishaji wa kina unaotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Hapa ni mahali pa majadiliano ya kina kati ya waamini wa dini mbali mbali pamoja na tamaduni zao.

Kwa njia ya elimu, Kanisa linapania kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu kati ya watu, maabara muhimu katika ujenzi wa ubinadamu mpya kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kongamano hili ni matunda ya changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliyewataka wajumbe wa Baraza la Elimu Katoliki kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya Tamko la Elimu Katoliki na Jubilei ya Miaka 25 ya Mwongozo wa kitume kuhusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazosimamiwa na Mama Kanisa. Maandalizi ya Kongamano hili yalianza kushika kasi kunako mwaka 2012 kwa kuandaa maswali dodoso kuhusiana na sekta ya elimu mintarafu: utambulisho na utume; walengwa wa elimu, malezi na changamoto.

Askofu mkuu Zani anaendelea kusema, mchakato wa elimu katoliki unajikita katika mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili mintarafu Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kuwapatia vijana wa kizazi kipya elimu itakayowasaidia kuwa raia wema pamoja na kuchangia ustawi na maendeleo ya jamii zao katika misingi ya haki, amani na maridhiano. Sekta ya elimu katika ulimwengu mamboleo inakabiliana na changamoto nyingi kwanza kabisa ni utambulisho wa shule au taasisi inayojikita katika msingi wa Injili; umuhimu wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu ili kupambana na mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema, mambo ambayo yanaendelea kusambaa kwa kasi utadhani ni moto wa mabua!

Mafungamano ya kijamii katika umoja na udugu; ukweli, haki na amani yako mashakani kutokana na ubinafsi. Changamoto kubwa iliyoko kwenye sekta ya elimu ni kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanapata nyenzo, ujuzi na maarifa ya kuweza kufikiri na kutenda, tayari kuleta mabadiliko ili kuitengeneza jamii kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kupambana na vishawishi vinavyotolewa na vyombo vya upashanaji habari vinavyotaka kuwatumbukiza katika ulaji wa kupindukia. Changamoto nyingine inayopaswa kufanyiwa kazi ni kuhakikisha kwamba, wanafunzi wanapokuwa shuleni wanapata nafasi ya elimu ya maisha ya kiroho, ili kuwajengea moyo wa uchaji wa Mungu, uzalendo na uwajibikaji. Wadau mbali mbali wa elimu wanapaswa kuendelezwa ili kukabiliana na kasi kubwa ya mabadiliko katika mfumo wa elimu katika jamii inayojengwa na wanafunzi kutoka katika tamaduni, imani na mataifa mbali mbali.

Askofu mkuu Angelo Vincenzo Zani anakaza kusema, changamoto ya elimu kwa vijana wa kizazi kipya ni kubwa sana na ndiyo maana Kanisa linapenda kuzivalia njuga changamoto hizi, ili kweli: shule, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki zinatekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya kweli za Kiinjili na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kanisa linaendelea kuhamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko, kutoka huko lilikojificha, tayari kutoka kimasomaso ili kuwajengea watu msingi wa majadiliano, umoja, udugu, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni muda muafaka wa kutangaza Injili ya matumaini badala ya kuelemewa na wasi wasi na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko! Hiki ni kipindi cha kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya uhuru wa elimu kwa wazazi kadiri ya Katiba na sheria za nchi husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.