Jumapili wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, katika hotuba yake fupi kwa mahujaji na wageni waliofika kumsikiliza katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Matakatifu Petro, , alielekeza hotuba zaidi katika masomo ya Jumapili, yaliyoashiria kukaribia kwa mwisho wa mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Masomo , yaliyogusia ufunuo katika ujio wa ufalme wa Mungu katika 'nyakati za mwisho'.
Tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko alilenga zaidi katika lengo la mwisho la maisha yetu hapa duniani, kwamba ni kukutana na Kristo Mfufuka. Papa alieleza huku akihoji ni wangapi ambao hufikiri juu ya hili? Na akasema tatizo si lini dalili za maonyo ya kinabii juu ya mwisho wa dunia lini zitaanza kuonekana, lakini hasa ni iwapo kweli tupo tayari kuukabili mwisho wa dunia. Na vivyo hivyo , tatizo si jinsi mwisho wa dunia utakavyotokea lakini hasa jinsi tunavyopaswa kuuishi wakati huo.
Papa alieleza na kutoa wito kwamba, tangu sasa tunatakiwa kuyaishi matukio hayo kama inavyopaswa kwamba ni kuyajenga maisha ya baadaye kwa utulivu, uaminifu na kumtumaini Mungu. Hata hivyo akaongeza, ingawa ni vigumu kuishi kwa matumaini , lakini inawezekana kwa kutazama kwa nguvu sura ya Kristo Mfufuka, kwa kuwa Yesu si tu hatima ya njia yetu ya hapa duniani , lakini ni Yeye Yesu mwenye we huongozana na sisi katika maisha yetu ya sasa kila siku, akitafuta kutuokoa na manabii wa uongo na mawazo maovu. Papa alieleza na kuwauliza waliokuwa wakimsikiliza ni wangapi wanategemea kuongoza na wapigabao au wapiga ramli, badala ya kuomba kuongozwa na Yesu, ambaye daima yumo katika kuliishi Neno lake lenye kuongoza na ambaye daima hubaki na sisi.
Baada ya hotuba yake, Papa aliwakumbuka wahanga wa shambulio la kigaidi lililotokea Paris Ufaransa siku ya Jumamosi, shambulio alilolitaja kuwa ni unyama wa hali ya juu.
Na baadaye , kwa njia ya telegramu , alipeleka salaam zake za rambirambi kwa Kardinali André Vingt-Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, akimhakikishia ukaribu wake kwa waathirika, familia zao na wafanyakazi wa dharura kwamba yuko pamoja nao katika maombi. Salaam hizi za Papa zilizotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican. Papa Francisko amelaani vikali vitendo vyote vya vurugu, na kumwomba Mungu neema ya kuhamasisha mawazo ya amani na mshikamano. Na amemwomba Mungu, Baba wa huruma, awapokee waathirika katika amani ya Nuru yake na kuwapa faraja na matumaini majeruhi wote na familia zao. Pia aliwataja wote walioshiriki katika kutoa msaada kwamba kwao wote yu karibu nao kiroho. Kwa mara nyingine tena, Papa alirudia kusema kwa nguvu kulaani vurugu, akisema , haiwezi kutatua jambo lolote.
All the contents on this site are copyrighted ©. |