2015-11-16 07:19:00

Mashambulizi ya kigaidi ni kufuru kwa Mungu na ni vitendo vya kinyama!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 15 Novemba 2015 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa mara nyingine tena ameonesha masikitiko yake kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza nchini Ufaransa. Watu zaidi ya 132 wamefariki dunia na wengine 350 wamepata majeraha makubwa. Magaidi 7 wamejilipua kwa mabomu.  Kwa usiku mzima, mji wa Paris uligeuka kuwa ni uwanja wa fujo na vurugu, kila mtu akijitahidi kukimbia mbali na kifo, ili kusalimisha maisha yake.

Baba Mtakatifu amelaani mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa kwa mwamvuli kwa jina la Mungu kuwa ni kufuru kubwa. Amechukua nafasi hii kulaani vitendo vyote vya kigaidi vinavyofanywa dhidi ya binadamu. Baba Mtakatifu amewaomba waamini kusali na kumwomba Bikira Maria aweze kuilinda Ufaransa na dunia nzima, asaidie kukuza na kudumisha mawazo ya huruma na amani kati ya watu.

Mapema siku ya Jumamosi, tarehe 14 Novemba 2015 Baba Mtakatifu Francisko alikaza kusema, mashambulizi ya kigaidi kamwe hayataweza kusaidia kutatua matatizo na changamoto zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Kwa sasa Kanisa linapenda kuelekeza mawazo yake kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na mashambulizi ya kigaidi huko Paris, Ufaransa; mashambulizi ambayo kimsingi yanatibua mafungamano ya kijamii, amani na utulivu miongoni mwa watu. Mashambulizi ya kigaidi ni kinyume kabisa cha utu wa binadamu na misingi ya kiimani.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahojiano na Bwana Lucio Brunelli, Mkurugenzi wa kituo cha Televisheni cha TV2000 kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi yaliyojitokeza usiku wa Ijumaa tarehe 13 Novemba 2015. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ameshtushwa na kusikitishwa sana na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Ni mashambulizi yanayofanywa na watu dhidi ya utu na heshima ya binadamu, jambo ambalo linakuwa ni vigumu sana kuingia kichwani mwake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hakuna sababu yoyote ile inayoweza kuhalalisha mashambulizi ya kigaidi. Kanisa linapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wananchi wote wa Ufaransa hasa wakati huu wanapoendelea kuomboleza kutokana na msiba mkubwa uliolikumba taifa lao. Hii ni sehemu ya vita kuu ya tatu ya dunia ambayo Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akiigusia katika hotuba zake mbali mbali. Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupinga vitendo vyote va kigaidi, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anaungana na Baba Mtakatifu Francisko katika sala kwa ajili ya kuwaombea wale wote waliopoteza maisha yao huko Ufaransa kutokana na vitendo vya kigaidi. Kanisa Katoliki nchini Italia limetolea sadaka ya nia ya misa kwa ajili ya kuwaombea marehemu na majeruhi waweze kupona haraka. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya za Kikristo kuendeleza mchakato wa mafungamano ya kijamii kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano na kamwe waamini wasitumbukie katika kishawishi cha woga na hofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.