2015-11-16 07:42:00

Burundi hali inaendelea kuwa tete! Vita ya wenyewe kwa wenyewe inanukia!


Vurugu, machafuko, kinzani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa nchini Burundi kiasi cha Jumuiya ya Kimataifa kuhofia kwamba, Burundi wakati wowote ule inaweza kutumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo litaleta maafa makubwa sana, ikiwa kama hatua za makusudi hazitachukuliwa mapema iwezekano. Hali tete ya kisiasa na kijamii nchini Burundi inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ushindi wa Rais Pierre Nkurunziza katika awamu ya tatu katika uchaguzi mkuu uliosusiwa na vyama vya upinzani mwezi Julai, kwa madai kwamba Rais Nkurunziza alikuwa amekiuka Katiba ya Burundi ambayo ni sheria mama, jambo ambalo linapingwa vikali na Rais mwenyewe!

Kwa upande mwingine machafuko haya ya kisiasa yamekuwa yakichochewa na mchezo mchafu wa ukabila kati ya Wahutu na Watusi, mchezo ambao kunako mwaka 1994 ulisababisha mauaji ya kijmbari nchini Rwanda. Rais Paul Kagame wa Rwanda hivi karibuni amewaonya wananchi wa Burundi kutotumbukia katika kishawishi cha ukabila na hatimaye kujikuta wakiogelea katika mauaji ya kimbari na badala yake wajifunze kwa dhati historia ya Rwanda, kwani zaidi ya watu laki nane walipoteza maisha.

Leo hii asilimia 85% ya wananchi wote wa Burundi ni Wahutu na asilimia 14% ni Watutsi. Inasikitisha kuona kwamba, Serikali ya Burundi iliyoko madarakani inaendelea kushuhudia wananchi wasio na hatia wakiendelea kupoteza maisha yao! Mkataba wa Arusha wa Mwaka 2000 ulikuwa umepiga rufuku kwa rais kuongoza nchi katika awamu tatu mfululizo anasema Padre Gabriele Ferrari ambaye kwa miaka mingi ameishi na kufanya utume wake nchini Burundi kama missionari. Kuna mauaji ya kinyama yanayoendelea kutendeka na watu wanashuhudia maiti zikiwa zimezagaa barabarani, kama onyo kwamba, hapa kuna hatari kubwa!

Taarifa zinaonesha kwamba, kutokana na hali kuwa tete nchini Burundi, Jumuiya ya Ulaya imeamua kuwaondoa wafanyakazi wake nchini Burundi na wale wanaobaki waangalie usalama wao. Serikali ya Burundi inaishutumu pia Serikali ya Ubelgiji kwa kuwapatia silaha wapinzani wake ili kuendeleza mchafuko nchini Burundi na kwamba, inapania tena kuitawala Burundi kwa kuwatumia wapinzani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.