2015-11-14 15:17:00

Wakimbizi si idadi tu, bali ni watu wenye sura, heshima na utu!


Shirika la Wayesuit la huduma kwa wakimbizi JRS linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwake, matunda ya taabu, mateso na nyanyaso alizokabiliana nazo Padre Pedro Arrupe, mkuu wa Shirika la Wayesuit alipokuwa nchini China na Kusini mwa nchi ya Vietnam. Ni kiongozi aliyeonja makali ya mabomu ya atomik kule Hiroshima pamoja na kushuhudia wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi waliokuwa wanatafuta hifadhi na usalama wa maisha. Akatambua kwamba, hii ilikuwa ni changamoto ambayo ilipaswa kuvaliwa njuga na Wayesuit katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa.

JRS ikaanzishwa ili kusikiliza kilio cha wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwahudumia kiroho na kimwili pamoja na kuhakikisha kwamba, haki zao msingi na utu wao kama binadamu vinalindwa na kudumishwa na wote. Hawa ni watu wanaopaswa kusikilizwa na kufarijiwa. Wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia leo hii ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa hususan Barani Ulaya. Inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi millioni sitini wanaoishi sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni idadi kubwa kuwahi kutokea tangu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Hawa ni watu wenye sura na majina; watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 14 Novemba 2015 alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Shirika la Wayesuit la huduma kwa wakimbizi. JRS inashirikiana kwa karibu zaidi na watawa pamoja na waamini walei katika kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwasindikiza, kuwahudumia na kutetea haki msingi za wakimbizi, mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Padre Arrupe katika huduma kwa wakimbizi.

JRS ni Shirika ambalo daima limekuwa makini kusoma alama za nyakati, tayari kuhudumia kwa weledi na umakini mkubwa katika maeneo mbali mbali yenye vita, migogoro na kinzani za kijami kama vile: Syria, Afghanstan, Jamhuri ya Afrika ya Kati pamoja na DRC. Watu wengi katika maeneo haya wanashiriki kikamilifu katika utume unaotolewa na JRS. Lengo ni kuwatangazia watu Injili ya matumaini kwa njia ya huduma ya elimu inayowapatia ujuzi na maarifa ya kuweza kuboresha hali ya maisha yao, tayari kuwa na kesho iliyo bora zaidi. Ni huduma inayowajengea wakimbizi hali ya kujiamini, ili kutumia vyema karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao msingi.

Watoto ambao wanalazimika kukimbia nchi zao anakaza kusema Baba Mtakatifu, elimu inakuwa ni mahali pa kufurahia uhuru na ulinzi unaotolewa kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni. Lakini inasikitisha kuona kwamba, shule nazo zimekuwa ni mahali pa fujo na vurugu na mara kwa mara zimekuwa zikishambuliwa. Shule zinapaswa kuwa kweli ni mahali pa majadiliano na madaraja ya watu kutoka katika kabila, lugha na jamaa wanapokutana, ili kupata elimu. Baba Mtakatifu anasema elimu inawasaidia watoto wa wakimbizi kutambua wito wao na hatimaye kukuza karama walizonazo, lakini bahati mbaya watoto na vijana kutoka kwenye kambi za wakimbizi hawana bahati ya kupewa elimu bora zaidi kwani wengi wanashindwa kuendelea na masomo ya shule za sekondari, tayari kuingia kwenye vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, JRS inapania kuwasaidia wakimbizi wanafunzi laki moja kupata elimu, ili kumwilisha kauli mbiu ya huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza wadau mbali mbali katika mchango wao wa hali na mali, ili kuhakikisha kwamba, JRS inafikia malengo yake. Heri wenye huruma maana watapata huruma. Na kwa maneno haya, Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa wajumbe wa JRS wanapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.