2015-11-14 08:40:00

Msalaba alama ya huruma na matumaini kwa wakimbizi na wahamiaji Lampedusa


Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba, Msalaba aliopewa zawadi na Rais RaĆ¹l Castro wa Cuba upelekwe na kuhifadhiwa Lampeduda, Kusini mwa Italia, mji ambao umekuwa ni kimbilio la matumaini kwa wakimbizi na wahamiaji wengi wanaotafuta hifadhi ya maisha Barani Ulaya. Uamuzi huu wa Baba Mtakatifu umetangazwa na Kardinali Francesco Montenegro, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Agrigento, Italia.

Huu ni Msalaba ambao umetengenezwa kutokana na mabaki ya mashua na merikebu zilizovunjika baharini, kumbu kumbu endelevu inayopaswa kujikita katika mioyo ya watu, ili waweze kuguswa na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora Barani Ulaya. Msalaba huu utakuwa ni kumbu kumbu ya upendo na heshima ambayo Baba Mtakatifu anaonesha daima kwa wakimbizi na wahamiaji, wanaopaswa kuonja huruma na upendo kutoka kwa nchi wahisani.

Kardinali Montenegro anasema, Baba Mtakatifu anawapenda na kuwaheshimu sana waamini wa Jimbo kuu la Agrigento kutokana na ushuhuda wao wa upendo kwa wahamiaji na wakimbizi, changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwajibika kikamilifu kulinda na kutetea utu, heshima na haki za wakimbizi na wahamiaji nchini Italia, jambo ambalo kwa sasa limekuwa ni kichokoo cha kampeni za uchaguzi kwa baadhi ya vyama nchini Italia, ili kuweza kujipatia kura kutokana na kuwajaza wananchi hofu juu ya usalama wao kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa sasa Barani Ulaya.

Itakumbukwa kwamba, kuna wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kufa maji katika kilindi cha bahari ya Mediterrania na wanasisa bado wanawaangalia kwa jicho la kengeza kiasi cha kushindwa kutekeleza hata yale maamuzi wanayoyafanya kwenye mikutano ya kimataifa! Kisiwa cha Lampedusa kwa sasa ni kielelezo cha kifo na matumaini kwa wahamiaji na wakimbizi wanaofanikiwa kuwasili nchini Italia.

Kardinali Montenegro anakaza kusema, Msalaba huu utatumika wakati wa kuzindua maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, katika maadhimisho ya Jumapili ya pili ya Kipindi cha Majilio. Msalaba huu utafanyiwa maandamano ya kiroho katika maeneo mbali mbali ya Jimbo kuu la Agrigento na baadaye utatunzwa kwenye Parokia ya Mtakatifu Gerlando, iliyoko Lampedusa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.