2015-11-14 09:49:00

Kongamano la Kimataifa la Elimu Katoliki kutimua vumbi 18-21 Novemba!


Kanisa Katoliki linapenda kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika mwono chanya na utambulisho wake katika sekta ya elimu, kwa kuonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko, unaojikita katika elimu makini inayopania kumpatia mwanadamu ukombozi kamili: kiroho na kimwili. Kanisa linataka kuondoka na mwelekeo wa kujitafuta na kujilinda, ili kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Haya ni mambo msingi yaliyobainishwa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki tarehe 13 Novemba 2015 kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano la Elimu Kimataifa, kuanzia tarehe 18 hadi 21 Novemba 2015. Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu Elimu ya Kikristo, “Gravissimum educationis” na Jubilei ya miaka 25 tangu Katiba ya kitume kuhusu Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za Kikatoliki, “Ex Corde Ecclesiae”  ilipochapishwa.

Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anapenda kujitosa kimasomaso katika mchakato wa elimu makini, ili kuweza kuwafunda barabara vijana wa kizazi kipya, tayari kukabiliana na changamoto za maisha, ili kuutengeneza ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Elimu ni ufunguo wa maisha ya binadamu na jamii katika ujumla wake. Katika ulimwengu mamboleo, sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto nyingi. Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki hivi karibuni lilituma maswali dodoso katika nchi 62 na majibu ya maswali haya kwa sasa yamehaririwa na kuwa ni sehemu ya hati ya kutendea kazi wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Elimu Katoliki Kimataifa.

Hati hii ya kutendea kazi inajikita kwa namna ya pekee katika: mchakato wa elimu makini, majiundo awali na endelevu; imani, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; ushuhuda kutoka katika maeneo ambayo hayana uhuru kamili kuhusiana na masuala ya uhuru wa kidini; wajibu wa kuzungumza ukweli katika uwazi pasi na woga; umuhimu wa elimu katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa jamii, hususan maskini, ili elimu iweze kuwapatia ukombozi wa kweli. Kanisa linatambua kwamba, elimu kimsingi ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu inayotekelezwa katika mchakato wa upendo kwa Mungu na jirani.

Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa kikamilifu ili hatimaye waweze kujikita katika elimu inayowajengea utamaduni wa watu kukutana na kushirikiana kwa dhati katika mchakato wa maendeleo endelevu anakaza kusema Professa Italo Fiorini, kutoka Chuo kikuu cha LUMSA kilichoko hapa mjini Roma, wakati alipokuwa anawasilisha maadhimisho ya Kongamano la Elimu Kimataifa mjini Vatican kwa waandishi wa Habari mjini Vatican.

Kanisa linataka kukuza majadiliano ya kina na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu pasi na kupoteza utambulisho wake na badala yake kuwa kweli ni kielelezo cha ushuhuda wa huduma ya upendo inayovunjilia mbali kuta zinazowatenganisha watu kwa sababu mbali mbali. Hivi ndivyo anavyofafanua Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki wakati wa kuwasilisha changamoto na umuhimu wa kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa kuwapatia elimu makini!

Vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki vinapaswa kuwa ni mahali pa ujenzi na ushuhuda wa upendo; mahali pa kutangaza na kumwilisha Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya uhalisia wa maisha. Jumuiya ya Chuo kikuu cha Kikatoliki iwe ni mashuhuda wa huduma ya upendo, majadiliano, heshima na kielelezo cha utambulisho wa imani inayomwilishwa katika matendo, tayari kuvunjilia mbali kuta za utengano kati ya watu! Chuo kikuu si mahali pa kupika majungu na kinzani za kijamii, bali ni eneo la kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili katika maisha ya watu, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ukombozi. Watu wanaweza kuwa na maoni na mielekeo tofauti katika maisha, lakini wote hawa wanaunganishwa na kufumbatwa na huduma na ushuhuda wa upendo!

Kwa upande wake, Askofu mkuu Angelo Vincenzo Zani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki anakaza kusema, tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vyuo vikuu na taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali duniani. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 95% ya shule za Kikatoliki. Leo hii kuna vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu 1860 na kati yake kuna vitivo vya masomo ya Kikanisa 500; Vyuo vikuu kwa sasa ni 1350. Taasisi zote hizi zinawahudumia wanafunzi takribani millioni kumi.

Kuna baadhi ya vyuo vikuu ambavyo vinapata ruzuku kutoka Serikalini na Kanisani na hivyo kuweza kutoa elimu ya bure, lakini idadi yake ni ndogo sana. Sehemu kubwa ni wanafunzi kuchangia katika elimu, ingawa sehemu kubwa ya gharama inachangiwa na Kanisa. Inasikitisha kuona kwamba, Kanisa nchini Italia katika kipindi cha miaka kumi iliyopita limejikuta likifunga shule zaidi ya 800 kutokana na kupanda kwa gharama ya uendeshaji.

Maadhimisho ya Kongamano la Elimu Kimataifa yatahitimishwa hapo tarehe 21 Novemba 2015 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, tayari kuanza mchakato mpya katika utekelezaji wa sera na mikakati ya elimu kwa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazoongozwa na Kanisa Katoliki. Itakuwa ni fursa ya kuanzisha Mwongozo wa jumla wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu za Kanisa Katoliki.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia uamuzi wa kuanzisha Mfuko wa Elimu Katoliki, kama sehemu ya kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Tamko kuhusu Elimu ya Kikristo. Ni mfuko unaopania kusaidia juhudi za tafiti pamoja na kuwajengea uwezo wanafunzi wanaoishi katika kambi za wakimbizi na wale wanaotoka katika familia maskini zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.