2015-11-14 16:16:00

Kanisa linaendelea na maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu licha ya vitisho


Padre Federico Lombardi Msemaji mkuu wa Vatican anasema wakati huu Jumuiya ya Kimataifa inapokabiliana na matatizo na changamoto za mashambulizi ya kigaidi na tabia ya watu kutaka kulipizana kisasi, kuna haja kwa waamini na wapenda amani wote duniani kushinda kishawishi cha woga usiokuwa na mashiko na badala yake kujikita katika huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuambata pia haki, amani na maridhiano kati ya watu!.

Wadau mbali mbali wahakikishe kwamba wanatekeleza dhamana kadiri ya na nafasi zao, ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Waamini hawana pamoja na watu wote wenye mapenzi mema hawana budi kuendeleza mchakato wa maisha yanayojikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu ni hitaji msingi kwa watu wa nyakati hizi na hili amelitambua Baba Mtakatifu Francisko!

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko wa kumwilisha upendo na huruma ya Mungu kati ya waja wake; tayari kuendeleza mchakato wa upatanisho, haki na amani, mahali ambapo bado kuna kilio kikubwa cha damu ya watu wasiokuwa na hatia! Hapa kuna haja ya kuondokana na kishawishi cha kukata na kukatishwa tamaa katika maisha kutokana na mashambulizi haya ya kigaidi ambayo kwa sasa yanaonekana kutaka kutikisa matumaini ya watu!

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema, huruma ya Mungu ni jibu makini kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waamini wakati wanapotembea katika giza la mashaka na wasi wasi, kama ilivyokuwa wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia; mashambulizi, dhuluma na nyanyaso kutoka kwa watala dhalimu. Misimamo mikali ya kidini inaendelea kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya watu kiasi hata cha kutaka kulipizana kisasi kwa misingi ya udini usiokuwa na mashiko wala mguso!

Padre Lombardi anakaza kusema, hata leo hii Baba Mtakatifu anapozungumzia kuhusu Vita kuu ya Tatu ya Dunia, bado kuna haja ya kutangaza na kushuhudia Ujumbe wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake, kwa kuambata ujasiri na upendo pasi na kukata tamaa! Huu si wakati wa kufuta maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu wala kuwa na wasi wasi isiyokuwa na msingi. Jambo muhimu ni kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama vinapewa kipaumbele cha pekee kwa watu na mali zao.

Waamini wanapaswa kuishi kipindi hiki kwa hekima na busara; kwa ujasiri, imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Watu wasonge mbele kwa imani na matumaini licha ya mashambuliz, chuki na uhasama unaopandikizwa miongoni mwa watu kutokana na imani na misimamo mikali ya kidini. Baba Mtakatifu Francisko analiongoza Kanisa na kuwataka waamini kuwa na imani kwa Roho Mtakatifu anayewaongoza na kuwaonesha dira na njia ya kupita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.