2015-11-14 17:07:00

Dr. Magufuli aanza kutema cheche za mageuzi Tanzania!


Watanzania wengi wanasema, Rais Magufuli ni kiongozi aliyechaguliwa kwa wakati muafaka kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya watanzania wengi. Akiungwa mkono na viongozi, wafanyakazi wa umma na watanzania katika ujumla wao, kweli Tanzania inaweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi na chachu ya maendeleo endelevu ukanda wa Afrika ya Mashariki. Siku chache za uongozi wake, cheche za mabadiliko nchini Tanzania zinaanza kujionesha kwa wafanyakazi kujituma na kuwajibika zaidi. Kasi hii ikiendelea pasi na kukoma, basi kiu ya watanzania wengi itakuwa imetulizwa kama anavyokaza kusema, Dr. John Pombe Magufuli, hapa ni kazi tu hadi kieleweke!

Wakati huo huo, Bwana Ban Ki-Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania. “Uchaguzi wa mwaka 2015 ni uthibitisho wa wazi na dhamira ya muda mrefu ya Watanzania kwa demokrasia, amani na utulivu. Nina imani kuwa masuala ya uchaguzi yaliyobakia yatashughulikiwa kupitia taratibu za kisheria zilizopo kwa njia ya amani na uwazi.” Bw. Ban Ki Moon amesema kwenye barua yake ya pongezi ambayo amemtumia Mhe. Rais Dkt. Magufuli.

Bw. Ban Ki-Moon amesema anaamini kuwa, chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli, Serikali ya Tanzania itashughulika na juhudi za kuondoa umaskini, kuimarisha utawala bora na kuendeleza juhudi za Tanzania katika kupigania amani na utulivu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na nje zaidi ya Ukanda huu. “Napenda kukuhakishia kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kukuunga mkono pamoja na Serikali yako katika juhudi hizi”. Mhe. Ban Ki Moon amesema. Katibu Mkuu Bw. Ban Ki-Moon pia ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenza imara na wa kutumainiwa na Umoja wa Mataifa kwa miongo yote. “Nathamini ushirikiano uliopo baina ya Umoja wa Mataifa na nchi yako na katika kuendeleza malengo ya UN, nakutakia mafanikio katika kutekeleza shughuli zako”. Bw. Ban Ki-Moon amesema katika salamu zake.

Na mwandishi maalum.


 








All the contents on this site are copyrighted ©.