2015-11-13 15:17:00

Msiabudu miungu wa uwongo!


Mwanadamu katika maisha yake mara nyingi anakumbana na kishawishi cha kutaka kujitengenezea miungu ya uwongo na kuiabudu na hata wakati mwingine, kuna baadhi ya mazoea yanageuzwa kuwa kama miungo wadogo kana kwamba, ni mambo ya kudumu milele. Waamini wanapaswa kutambua kwamba Mwenyezi Mungu ndiye uzuri wa milele ambao mwanadamu anapaswa kuutafuta na kuuambata katika maisha yake. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 13 Novemba 2015.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mzaburi anaimba kwamba Mbingu zahubiri utukufu wa Mungu na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Lakini kwa bahati mbaya mwanadamu kwa kiasi kikubwa ameshindwa kutambua na kukiri utukufu wa Mungu unaojionesha katika kazi ya mikono yake na matokeo yake, binadamu amegeuza kazi hii kuwa ndiyo miungu wake na kusahau kwamba, iko siku itapotea na kutoweka katika uso wa nchi.

Baba Mtakatifu anasema, hata mwamini asipokuwa makini anaweza kutumbukia katika kishawishi cha kutukuza na kuabudu kazi ya mikono ya Mwenyezi Mungu na kushindwa kumwendea Mungu aliye asili ya mambo yote haya. Hiki ni kishawishi cha kuabudu mambo yanayoonekana machoni pa watu, bila kuvuka ili kumwendea Mwenyezi Mungu mwenyewe. Mwanadamu anayakumbatia haya kutokana na nguvu na nishati inayozalishwa nayo, lakini hawana nafasi ya uwepo wa Mungu ambaye ni Muumbaji wa vyote vinavyoonekana na vile visivyoonekana.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mazoea yanaweza kuwa ni miungu wadogo kama ambayo Yesu mwenyewe amefafanua kwa kina na mapana katika Injili ya siku, kwamba watu walikuwa wanakula na kunywa, walikuwa wakiuza na kununua; wakioa na kuolewa na kusahau kwamba, yote haya yana mwisho wake! Lakini Mwenyezi Mungu ni wa milele! Huu ni mwaliko kwa waamini kuangalia uzuri usiochakaa wala kufutika machoni pa watu. Waamini wakati huu wanaalikwa na Mama Kanisa kuwa macho na mambo ya dunia, Kanisa linapokaribia kuufunga mwaka wa Liturujia. Iwe ni fursa ya kutazama na kutafakari uzuri na ukuu wa Mungu unaojionesha katika kazi ya uumbaji, tayari kumtolea Mungu sifa na shukrani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.