2015-11-13 07:13:00

Leo ni patashika nguo kuchanika!


Wakati fulani Wataalamu wa Hali ya Hewa wanatabiri mabadiliko ya kutisha ya hewa, kama vile gharika ya El nino, au mvua za radi,  upepo mkali. Kadhalika Wataalamu wa mwendo wa ardhi wanatabiri matetemeko ya nchi, na wale wa mwendo wa hali ya Bahari wanatabiri dhoruba na mawimbi baharini. Mara nyingi madhara yatokanayo na utabiri huo ni majanga mazito yanayoweza kubadili kabisa mazingira yaliyoathirika. Mathalani gharika hubomoa makao na kuacha ukiwa. Mmomonyoko wa udongo huhamisha sehemu kubwa ya ardhi. Mafuriko ya maji huvunja na kusomba ovyo madaraja. Kunatokea pia mlipuko wa magonjwa ya ajabu, watu na wanyama hupoteza uhai nk. Kwa hiyo majanga hayo yanatufunulia hali mpya ambayo haikuwepo kabla. Tunaweza kuyaita ni Ufunuo wa ukurasa au sura mpya ya dunia.

Neno hili Ufunuo au kwa kiingereza apocalypse ni la kigiriki apokalipto lenye maneno mawili: apo ni kuonesha, kufichua au kufunua na kalipto ni kuficha, kufunika, kufunga, kugubika kama chungu kilichofunikwa au kufungua pazia lililofunga ukumbi, au kufunua kope zilizoziba macho. Kwa hiyo Apokalipto ni kufunua kitu kilichofunikwa, kufungua macho yaliyofumbwa, au kufichua kitu kilichofichwa nk.

Leo tutasikia utabili wa maangamizi makuu ya ulimwengu na ufunuo wake. Lakini kabla ya kuyasikia maangamizi hayo, unatahadharishwa kabla kuwa: “asomaye na afahamu” (Mk 13:14). Kwa hiyo ili kuelewa sawasa utabiri wa majanga hayo na ufunuo wake, yatubidi kwanza kuelewa mazingira yake. Injili ya Marko iliandikwa mwaka 68 baaada ya Kristu, wakati huo Yerusalemu ilikuwa bado kubomolewa, lakini tayari mizengwe na vurugu mechi zilishaanza. Kadhalika kipindi hicho madhulumu ya Nero yalikuwa yanaishaisha, lakini kulikuwa bado na fujo za mauaji. Halafu baada ya kifo cha Nero kukazuka vita vya Warumi wenyewe kwa wenyewe. Uyahudini nako hakukuwa kumetulia kwani nako kulikuwa na migomo ya hapa na pale iliyoambatana na njaa na milipuko ya magonjwa yaliyoua watu na wanyama. Majanga haya yakawa giza nene lililogubika akili na mioyo ya watu, wakabaki kuduwaa na wasielewe ulimwengu unaelekea wapi. Kwa wenzangu wakristu hao ndiyo walishindwa kabisa kuunganisha majanga hayo na matumaini yaliyoahidiwa na kutangazwa na mahubiri ya Yesu. Mapato yake ukazusha unabii mwingine, kwamba majanga hayo yalikuwa ni “mvua za rasharasha,” kwani kinafuata kiyama yaani mwisho wa dunia. Ama kweli, “Asomaye na afahamu.”

Utabiri tutakaousikia leo una lengo la kutufunulia pazia la ukumbi wa ukweli au kufungua kope za macho ili kuona mwanga mpya uliojificha katika majanga hayo. Kuonesha kwamba ni ufunuo wa ulimwengu mpya, Yesu anatumia lugha ya uzazi anaposema: “ujue huo ndiyo mwanzo wa utungu.” (Mk. 13:8). Maneno haya, “Mwanzo wa utungu,” yanaweza kufasiriwa kama mwanzo wa mateso makali, yanayotegemewa kufika. Ufasiri huo ni potovu. Kumbe, utungu ni maumivu makali sana anayopata mama anapokaribia kuzaa mtoto. Kwa hiyo “mwanzo wa utungu” ni maumivu makali kabla ya kuzaliwa ulimwengu mpya. Jamani, “Asomaye na afahamu.” Kadhalika “Baada ya dhiki hiyo” (Mk. 13:24) ni lugha ya ufunuo yaani baada ya kuangamizwa kwa Yerusalemu, kutazaliwa mwanzo mpya.

Halafu, “Jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake,” ni lugha ya ufunuo kutoka nabii Isaya: “Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.”(Isa. 13:10) Hapa Nyota za angani na matangamano yaani constellations zake ni picha ya ufunuo inayomaanisha nguvu na nuru inayotawala hapa duniani. Utawala wa Farao na watoto wake uliwakilishwa na jua, mwezi na nyota vilivyoabudiwa kama miungu. Miungu hiyo ilitoa nguvu kwa Mafarao wa Misri na wafalme wa Persia, Babilonia na Syria. Manabii walitabiri kuwa watawala hao – jua, mwezi, nyota na matangamano yake hazitabaki huko angani bali zitaanguka yatatiwa giza na hayatatoa mwanga wake tena yaani hazitaabudiwa tena. Huu ni ufunuo mpya wa matumaini na furaha. “Asomaye na afahamu.”

Yesu anaendelea kutabiri, juu ya kuanguka kwa mamlaka hayo anaposema: “nguvu zilizo mbinguni zitayumba.” Nguvu ya miungu iliyowapa wafalme mamlaka ya kukandamiza raia wao ikitikisika hapo kutakuwa mwanzo mpya wa ushindi. Halafu anasema: “Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu.” Mwana wa Adamu ni mtu mwenye utu wa kibinadamu tofauti na watawala wanaowakilishwa katika biblia kitabu cha Daniel kwa picha za wanyama wakali na wanaotisha. Belshaza Mfalme wa Babeli anawakilishwa kwa picha ya Simba jike. Mfalme wa Medi anawakilishwa kwa picha ya dubu. Halafu mfalme wa Persia ni picha ya Chui mwenye mabawa manne kama tausi na vichwa vinne. Wafalme waliotawala Palestina, hawana majina bali wanaoneshwa kuwa na meno ya chuma (Daniel  7:3-7). Wafalme hawa wote walikuwa wanyama watupu, hakuna aliyekuwa na utu au ubinadamu. Daniele anasema, baada ya utawala huo wa kinyama utatokea utawala wa mtoto wa binadamu mwenye utu (Daniel 7:8). Mungu anamkabidhi binadamu huyu, utawala ambao hautakuwa na mwisho. Huu ni ufunuo wa ujumbe wa matumaini, wa furaha, na ni mwanzo wa hali mpya, na mwanzo wa jumuia mpya ya Kiinjili ya kweli. “Asomaye na afahamu”.

Kisha Yesu anasema: “Ndipo atakapowatuma Malaika na kuwakusanya wateule wake.” Malaika hawa wanamaanisha mshenga. Kila mmoja anayekuwa chombo katika mikono ya Mungu na katika ukombozi wa Mungu, huyo ni malaika. Kwa hiyo endapo wakati fulani tunagubikwa na wingu la majanga mazito ya njaa, vita, madhulumu yanayokatisha matumaini jamii kiasi cha kuhatarisha maisha kwa migomo na kuhiari kufa, au kwa  wafuasi wa Kristo wanapopumbazika hadi kupoteza mwelekeo wa imani, au hata kwa mtu binafsi kiasi cha kutaka kujinyonga; Basi ndugu yangu, majanga ni ufunuo hivi yabidi kuyatafakari kwa makini ili kufahamu yanatufunulia nini. “Asomaye na afahamu”

Aidha katika kipindi cha kukata tamaa Yesu anatutumia malaika wake yaani wanapatikana Wakristo wema na waaminifu waaminifu wanaoweza kututuliza na kutuunganisha na wateule wake. Hao ndiyo malaika wetu. Yesu anatutuliza anapotualika kuuangalia na kuuiga mtini jinsi unavyokuwa upya. “Kwa mtini jifunzeni mfano: tawi lake huwa laini, na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno ni karibu; nanyi kadhalika, myaonapo mambo hayo yanaanza, tambueni ya kuwa yu karibu mlangoni.” Tunaalikwa daima kusoma ishara za nyakati na kwamba matendo yale yanayoonekana kuwa machungu sana katika maisha tuyatambue kuwa ni nafasi za mpito na ni ufunuo wa maisha mapya. “Asomaye na afahamu.”

Yesu anahitimisha vyema anaposema: “Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatimie.” Hapa anarejea kwenye tendo la Pasaka, pale jua lililopatwa giza, kulipokuwa na mtetemeko wa nchi kutokana na kuteswa kwa Yesu hadi kufa msalabani. Kulionekana kuwa ni janga kuu, kumbe hapo nguvu za kibinadamu zilianguka na ukafunuliwa mwanzo mpya yaani ufufuko. Haya ndugu yangu “asomaye na afahamu.”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.