2015-11-12 07:25:00

Watu wana njaa na kiu ya upendo, maisha, umoja, tunza, huruma na msamaha!


Baraza la maaskofu Katoliki India kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Novemba 2015 linaadhimisha Kongamano la Ekaristi Kitaifa, tukio linalohudhuriwa na Kardinali Malcolm Ranjith, mjumbe maalum wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya. Kuna Makardinali wanne, Maaskofu 71 na wajumbe 665 kutoka Majimbo mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini India. Kongamano hili linaongozwa na kauli mbiu “Kwa kushibishwa na upendo wa Kristo waweze kuwashibisha wengine”.

Katika maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe kwa njia ya video, wakati huu wanapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Kongamano la Ekaristi Takatifu kitaifa, hapo mwaka 1964 na kuhudhuriwa na Mwenyeheri Paulo VI. Maadhimisho ya Mwaka huu yanakwenda sanjari na maandalizi ya uzinduzi wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Maadhimisho haya ni zawadi kubwa ya Mungu kwa Kanisa na India katika ujumla wake, katika mchakato wa ukweli unaotafuta: matakatifu, mema na mazuri.

Mwenyeheri Paulo VI kunako mwaka 1964 alisema kwamba, Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya uwepo wa Kristo na upendo wa Mungu kati ya watu wake; upendo usiokuwa na kikomo uliojionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya mateso na kifo Msalabani. Upendo wa Kristo ni endelevu na unajikita katika maisha na mioyo ya watu na kwamba anawapenda watu wote wa India bila ubaguzi; watu ambao wamebahatika kumfahamu na kuonja upendo wake, chemchemi ya upendo na majitoleo kwa jirani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanamwilisha Agano linalowatakatifuza, kuwatakasa na kuwaunganisha waamini pamoja na Mungu wao. Ekaristi takatifu si chakula cha wenye nguvu, bali pia ni chakula kwa wanyonge na maskini. Ni kwa njia ya msamaha, waamini wanaweza kusonga mbele katika hija ya maisha yao ya kiroho.

Binadamu leo hii wanahitaji lishe bora ili kuzima njaa ya mwili. Lakini pia watu wana kiu na njaa ya upendo, maisha ya uzima wa milele, umoja, tunza, huruma na msamaha. Njaa hii inaweza kuzimwa na Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, Yesu Kristo aliyejimimina ili kuwakirimia watu maisha ya uzima wa milele. Mwili na Damu Azizi ya Yesu ni kielelezo cha msamaha wa dhambi za binadamu; msamaha unaojikita katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza kwamba, Ekaristi Takatifu inawawezesha waamini kujenga umoja na mshikamano na jirani zao, tayari kuguswa, ili hatimaye kujitahidi kutafuta suluhu dhidi ya baa la njaa linaloendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Ni mwaliko wa kuwatangazia watu waliokata tamaa Injili ya matumaini; kwa kujikita katika hija ya huduma, kushirikishana na kugawana hata kile kidogo walicho nacho waamini na kwa njia ya nguvu ya Mungu anaweza kufanya muujiza wa kugeuza umaskini huu kuwa kweli ni chemchemi ya utajiri. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Kitaifa yatakuwa ni mwanga wa furaha na matumaini kwa wananchi wa India; kikolezo cha: upendo,  umoja na mshikamano, tayari kuambatana na Bikira Maria ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa mambo makuu ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia na kuwatendea wananchi wa India.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.