2015-11-12 14:49:00

Waamini walei Injilisheni na kuyatakatifuza malimwengu!


Mwenyeheri Paulo VI alipokuwa anahitimisha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita alisema kwamba, hili ni tukio la upendo kwa Mungu, Kanisa na kwa Ulimwengu. Mababa wa Mtaguso wakawa na ujasiri wa kupembua kwa kina na mapana wito na maisha ya waamini walei ndani ya Kanisa na katika ulimwengu; mambo yanayojikita katika  Waraka juu ya Fumbo la Kanisa, “Lumen gentium” na Waraka kuhusu Kanisa na Ulimwengu, “Gaudium et spes”. Hizi ni nyaraka ambazo kwa namna ya pekee kabisa zinaweka msingi wa uelewa wa waamini walei na Taifa la Mungu katika ujumla wake.

Hapa kila mwamini anatekeleza dhamana na utume wake kadiri ya wito na nafasi yake ndani ya Kanisa kwa kushiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanatambua na kuheshimu wito na utume wa waamini walei katika Kanisa, kama wafuasi wa Kristo, tayari kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya Injili. Waamini walei wawe ni vyombo  na mwanga wa matumaini waliyopokea kutoka kwa Yesu, tayari kuganga madonda na mapungufu ya maisha ya mwanadamu kadiri ya sheria ya Mungu na maisha ya hapa duniani.

Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la waamini walei, wakati huu Mama Kanisa apoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu utume wa waamini walei, “Apostolicam actuositatem”. Tukio hili linaadhimishwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la waamini walei pamoja na Chuo Kikuu cha Santa Croce, kilichoko hapa mjini Roma.

Waraka huu unapembua kwa kina na mapana asili na wito wa waamini walei ambao wanahamasishwa na Mama Kanisa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Injili kwani hii ni dhamana ambayo wamejitwalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Waamini walei ni msada mkubwa katika kuhamasisha maisha ya Kikristo duniani na kwamba, wao wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuinjilisha na kuyatakatifuza malimwengu.

Ni Waraka unaotoa kipaumbele cha pekee katika majiundo kwa waamini na uwajibikaji wa pamoja kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican umefungua ukurasa mpya katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni wakati wa kuvuna matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakati huu Mama Kanisa anapoyaanza mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.