2015-11-12 15:06:00

Changamoto za kimissionari na Sheria za Kanisa!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hotuba yake kwenye Chuo kikuu cha San Damaso, kilichoko nchini Hispania, Jumatatu tarehe 10 Novemba 2015 amekumbusha kwamba, ni wajibu na dhamana ya Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kwa kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu kutoka katika Makanisa mahalia pamoja na Maaskofu wa Majimbo kwenye nchi za Kimissionari kuhakikisha kwamba: yanakuwa na miundo mbinu na rasilimali watu watakaosaidia mchakato wa ujenzi wa Kanisa, utekelezaji wa shughuli za kichungaji pamoja na kuendelea kutoa haki, chachu muhimu sana ya amani na utulivu kati ya watu.

Kardinali Filoni ameyasema haya wakati wa hotuba yake kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Nyaraka kuhusu: Upendo mkamilifu, “Perfectae caritatis” unaojikita katika upyaishaji wa maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa na Umissionari wa Kanisa “Ad Gentes”. Kumbu kumbu hii iliandaliwa na Kitivo cha Sheria za Kanisa, Chuo kikuu cha San Damaso. Ametumia nafasi hii kufafanua kuhusu sheria za Makanisa mahalia na shughuli za kimissionari kuanzia karne ya kumi na mbili, wakati ambapo Wamissionari walipewa upendeleo wa pekee kuhusiana na sheria za Kanisa.

Baraza la Kipapa linasema, leo hii kuna Majimbo makuu 186, Majimbo 785, Vikarieti za kitume 82 na maeneo ya kitume 32. Kuna majimbo ya kitume 4 na majimbo yanayojitegemea kisheria kwa sasa ni 6 pamoja na abasia moja ya kieneo, bila kusahau majimbo 6 ya Kijeshi. Ukweli huu wa mambo unaonesha jinsi ambavyo ni vigumu kuweza kutekeleza Sheria za Kanisa katika hali kama hii bila kuonesha utofauti wake, ndiyo maana bado Kanisa linaendelea kutoa upendeleo wa pekee kwa baadhi ya maeneo kama alivyoagiza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2005. Lengo ni kuyawezesha Makanisa mahalia kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kujikita katika upendo na neema ya kutangaza Injili ya Kristo kwa umakini mkubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.