2015-11-11 15:18:00

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa!


Kardinali Giuseppe Betori, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Firenza, Italia akimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu, wakati wa kongamano la Kanisa Katoliki Italia, Jumanne, tarehe 10 Novemba 2015 amesema, adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha, utume na umoja wa Kanisa. Ni mahali pa kuweza kukutana na kumpokea Yesu kristo katika Neno na katika Ekaristi Takatifu, ili kuambata utajiri unaobubujika kwa kukutana na Yesu katika hija ya maisha ya kiroho.

Kardinali Betori amewataja watakatifu waliolipamba Jimbo kuu la Firenze katika historia na maisha yake; hawa wakawa kweli ni mashuhuda wa imani tendaji; kielelezo cha viongozi wa Kanisa waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kristo. Ni mashuhuda wa imani waliosimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; wakawa ni mahuhuda na vyombo vya upendo kwa Mungu na jirani; Manabii na watetezi wa haki na amani. Ni waamini waliojipambanua katika elimu kama urithi na utajiri mkubwa kwa maisha ya mwanadamu pamoja na kuendelea kuwa kweli waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Jimbo kuu la Firenze limemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko umoja na mshikamano wake katika kuliongoza Kanisa la Kristo, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wanapenda kuendelea kuwasaidia wale wote wanaotafuta kuambata utu mpya, ukweli, uzuri na huduma ya upendo kwa jirani. Ni wajibu wa Kanisa kutangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha ya binadamu, kwa njia ya upendo na mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.