2015-11-11 15:05:00

Bosnia na Erzegovina kuna mazuri mengi ya kujifunza kutoka kwenu!


Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 11 Novemba 2015 kabla ya kutoa Katekesi kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amekutana na kuzungumza na Rais DraganĀ  Covic wa Bosnia na Erzegovina pamoja na ujumbe wake kwenye Ofisi ndogo iliyoko kwenye Ukumbi wa Paulo VI. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa uwepo wao mjini Vatican na kwamba, anaendelea kutunza ndani mwake mambo mema na mazuri ambayo amejifunza kutoka kwao!

Kwanza kabisa na watu ambao wameteseka sana; lakini wamekuwa tayari kuanza mchakato wa kusamahe na safari ya pamoja inayopania kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa kwa kushirikiana na kuendelea kujikita katika majadiliano. Baba Mtakatifu amemtaka Rais Covic kumfikishia salam na matashi mema kwa viongozi na wananchi wote wa Bosnia na Erzegovina. Anawasihi kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi nchini mwao, kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana na huduma kwa nchi yao.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwataka kuendeleza mchakato wa majadiliano, ili kuiwezesha nchi kusonga mbele! Anawakumbuka kwa namna ya pekee, vijana na maswali waliyomuuliza wakati alipowatembelea na bado anaendelea kuwaomba ili waweze kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.