2015-11-10 08:57:00

Simameni kidete katika ukweli na haki; pambaneni na saratani ya rushwa!


Baba Mtakatifu Francisko ameanza hija yake Jimbo kuu la Firenze ili kuhudhuria kongamano la tano ya Kikanisa nchini Italia kwa kutembmelea Jimbo Katoliki la Prato pamoja na kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi mapema asubuhi, Jumanne, tarehe 10 Novemba 2015. Baba Mtakatifu anasema, anatembelea mji wa Prato kama hujaji wa imani katika mji ambao uko chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa tayari kuanza hija ya maisha ya kiroho kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kwenye Agano la Kale.

Hii ni changamoto ya kutoka katika undani wao, tayari kukutana na kuwashirikisha wengine ile furaha na imani ya kuwa wamekutana na Yesu Kristo, Bwana na Mwalimu. Hiki ni kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, tayari kuendeleza mapambano kwa ujasiri unaojikita katika Maandiko Matakatifu pamoja na ari ya kimissionari, kwani kama Familia ya Mungu wanao wajibu mkubwa mbele yao. Ni dhamana ya Mama Kanisa kuwasindikiza wale waliopoteza njia kwa kuwajengea matumaini pamoja na kuwaganga na kuwaponya wale waliojeruhiwa kiasi cha kukata tamaa katika maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yesu Kristo, siku ile iliyotangulia kuteswa kwake aliowaonesha wafuasi wake kielelezo cha upendo mkamilifu unaojikita katika huduma kwa kuwaosha miguu, kielelezo cha kuwakumbatia wote pasi na ubaguzi. Baba Mtakatifu anawashukuru wananchi wa Prato kwa kuonesha umoja, mshikamano na upendo na watu kutoka katika tamaduni mbali mbali wanaoishi mjini hapo, kiasi cha kwenda kinyume na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Kwa njia ya upendo na mshikamano, wanaweza kuzisaidia familia zinazoogelea katika shida na mahangaiko mbali mbali na kamwe wasikatishwe tamaa na matatizo pamoja na changamoto wanazokutana nazo katika maisha, bali waendelee kujenga umoja unaowaweka karibu zaidi. Ili kutekeleza dhamana hii katika safari ya maisha yao ya kila siku wanapaswa kujivika fadhila ili kupambana na roho mbaya. Waamini wajivike fadhila ya ukweli na uwazi ili kujenga na kudumisha jamii inayojikita katika haki na uaminifu.

Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu yanapaswa kuheshimiwa, kutunzwa na kupata kazi inayolingana na binadamu. Amewakumbuka wananchi saba kutoka China waliofariki dunia kwa kuungua moto kwenye eneo la viwanda Prato, yapata miaka miwili iliyopita, kielelezo cha unyonyaji wa wafanyakazi. Jamii inachangamotishwa kupambana na saratani ya rushwa inayokinzana na utawala wa sheria, daima wananchi wajitahidi kusimama kidete kutetea ukweli. Vijana kamwe wasikate tamaa bali waendelee kusonga mbele kwa imani na matumaini; waamini wasikose kumkimbilia Bikira Maria wakati wa shida na raha, ili aweze kuwasaidia na kuwafariji na kambwa Yesu Kristo ataendelea kupandikiza ndani mwao mbegu ya matumaini na kamwe hawatahaidika. Amewashukuru vijana kwa kukesha na kusali kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huu hapo Jimboni Prato.

Kwa upande wake, Askofu Franco Agostinelli wa Jimbo Katoliki la Prato, amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kutembelea Jimbo Katoliki la Prato mji ambao unajipambanua kwa kuwa na watu kutoka ndani na nje ya Italia wanaofanya kazi, kwa kutegemeana, katika hali ya mshikamano na upendo wa maisha ya kiroho. Hii ni Jumuiya yenye mambo mengi ya kujivunia, lakini pia ina madonda na magumu yake; kwa namna ya pekee changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji.

Askofu Agostineli anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia pamoja na kutangaza Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Wataendelea kumuunga mkono katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, huku wakijitahidi kuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha na huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.