2015-11-10 14:57:00

Makongamano ya Kikanisa ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican


Kardinali Angelo Bagnasco Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, akimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na wajumbe wa Kongamano la Kikanisa nchini Italia, Jumanne, tarehe 10 Novemba 2015 kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria del Fiore amesema kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican umekuwa ni chachu ya kuibuka kwa makongamano ya Kanisa kitaifa nchini Italia, jambo ambalo limeiwezesha Familia ya Mungu kushikamana katika ushuhuda pamoja na kuendeleza mchakato wa kuipyaisha jamii.

Makongamano haya yamelisaidia Kanisa kupata utambulisho wake pamoja na kuendelea kutambua dhamana ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, hususan miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote waweze kupata nafasi ya kukutana na Yesu anayeponya na kuganga ubinadamu wao. Kanisa nchini Italia katika maadhimisho ya Kongamano hili la kimataifa linataka kwa namna ya pekee kabisa kutoka katika undani wake, kutangaza, kuambata historia, kuelimisha na kuleta mabadiliko katika imani.

Mambo haya anakaza kusema Kardinali Bagnasco yanajikita katika tafakari ya kina kuhusu utu wa binadamu kwa kuangalia hali halisi inayowakabili wananchi wa Italia kwa nyakati hizi. Lengo ni kuwajengea vijana wa kizazi kipya matumaini pamoja na kuendelea kukabilia na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa kwa kufanya rejea kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe, kielelezo cha utimilifu wa binadamu kinachokumbatia ekolojia ya binadamu  kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato si!

Kanisa Katoliki nchini Italia linataka kuonesha uso wa huruma kwa binadamu; Yesu Kristo anayewachangamotisha watu kuishi kwa pamoja katika umoja, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Kongamano hili linataka pamoja na mambo mengine kuimarisha ushirikiano na mshikamano kati ya wadau mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia, hususan katika sekta ya elimu kwa kuanzia katika familia na shule.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linamshukuru kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu kwa maneno, kwa kuwasikiliza pamoja na kuonesha ushuhuda wa kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuliambia Kanisa. Wanamshukuru kwa kuhimiza umuhimu wa Kanisa mahalia kujikita katika hija ya pamoja kama Sinodi, kama kielelezo cha umoja na utofauti miongoni mwa Familia ya Mungu nchini Italia. Maaskofu wanaendelea kumhakikishia Baba Mtakatifu utii na uwepo wao wa karibu katika maisha na utume wake kwa Kanisa la Kristo hasa wakati huu anapokabiliwa na changamoto kubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.