2015-11-10 14:39:00

Epukeni vishawishi, shuhudieni Injili ya furaha na huduma kwa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe wanaohudhuria kongamano la tano la Kikanisa nchini Italia, Jumanne, tarehe 10 Novemba akiwa kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Firenze amekazia umuhimu wa waamini kujikita katika utu mpya unaomwambata Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia, ili waweze kupata uzima wa milele.

Yesu ni kielelezo cha sura ya binadamu ambaye amejeruhiwa kwa dhambi, mapungufu na magumu ya maisha anayokumbana nayo katika hija ya maisha yake ya kila siku. Huu ni mwaliko wa kuangalia uso wa huruma wa Yesu aliyetesewa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu na kwa njia hii wataweza kumfahamu kwa undani kuwa Yesu ni nani! Yeye ni Mungu aliyetwaa sura na binadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ili kumkirimia mwanadamu utu mpya kadiri ya vionjo na maelekeo ya Yesu mwenyewe, kwa kuambata fadhila ya unyenyekevu.

Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Yesu Kristo alijitwalia hali ya binadamu katika mambo yote akawa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi. Utu na heshima ya mtu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kuachana na ubinafsi. Waamini wanapaswa kuambata imani kama chachu ya ya mabadiliko katika maisha ya mwanadamu mintarafu Injili ya Kristo na uwezo wa mwamini kujisadaka na kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza. Heri za Mlimani ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu yanayojikita katika mshikamano, sadaka, upendo pamoja na kujiaminisha katika huruma na upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ikiwa kama waamini watazingatia mambo haya wataweza kupata furaha ya kweli na maisha ya uzima wa milele, lakini daima wajitahidi kuwa na moyo wazi, tayari kuendeleza ujenzi wa urafiki na Yesu Kristo kwa kutambua nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa liwe na ujasiri kutoka ndani mwake, tayari kuwaendea watu huko waliko kuliko kuendelea kujifungua ndani mwake na kujitafuta lenyewe.

Baba Mtakatifu anasema, kuna vishawishi vingi ambavyo vinapaswa kushughulikiwa na Kanisa na kati yake ni kukabiliana na mafundisho potofu yanayojikita katika hali ya Kanisa kujiamini kupita kiasi na kushindwa kujikita katika utakatifu, unyenyekevu na kujisadaka. Badala yake, Kanisa linajiamini kwa kuwa na miundo mbinu madhubuti, kwa kujikita katika mtindo wa kudhibiti na wakati mwingine kuwa ni wagumu wa mioyo hata kujisikia kuwa ni bora zaidi kuliko wengine.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Mafundisho ya Kanisa ni hai, yanaonya na kuponya; yanajikita katika sura na mwili wa Kristo Yesu, ili yaweze kukua na kuongezeka. Kanisa halina budi kujipyaisha daima ili kuweza kukabiliana na changamoto katika maisha na utume wake kwa nyakati hizi; liwe tayari kubadilika kwa ajili ya kuwatetea na kuwasimamia wanyonge kama alivyofanya Mtume Paulo, mwalimu wa mataifa.

Baba Mtakatifu anasema, kishawishi cha pili kinajikita katika mafundisho ya uzushi yanayoonesha ubaridi, kutopea kwa imani na kukuza malimwengu. Lakini kinyume chake ni kufumbata Fumbo la Umwilisho ambalo ni msingi wa Mafundisho ya Kikristo pamoja na kuendelea kuiga mfano wa watakatifu ambao Kanisa nchini Italia, limebahatika kuwa na umati mkubwa wa waombezi na mifano bora ya kuigwa. Hawa ni watu waliokita maisha yao katika: Sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Ni watu walionesha mshikamano na maskini pamoja na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa hakika ni watu walioshikamana na waamini katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anaialika Familia ya Mungu nchini Italia kufanya maamuzi ya pamoja kwa kumwangalia Yesu Kristo, na kuwahudumia maskini kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama majibu muafaka wakati wa hukumu ya mwisho, ili hatimaye, kuingia katika ufalme wa Mungu na maisha ya uzima wa milele. Ikumbukwe kwamba, upendo kwa Mungu na jirani ni kipimo cha upendo wa Kikristo kitakachowawezesha waamini kushiriki furaha ya Kristo huko mbinguni!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kuwa kweli ni wachungaji, chemchemi ya furaha katika maisha na utume wao; watu wanaojikita katika sala na kwamba, waamini wao wawe ni nguzo imara katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Wawe ni wahubiri mahiri wa Injili ya Kristo na kushuhudia upendo kwa Mungu, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Upendeleo kwa maskini ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Kikristo.

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa nchini Italia kuondokana na uchu wa mali na madaraka, kwa kuwatumikia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kuambata ufukara wa Kiinjili unaounda, unaokarimu, unao enzi na kusheheni matumaini. Huduma ya Kanisa iwaguse na kuwafikia watoto wadogo wanaotelekezwa na kuishi katika mazingira hatarishi. Kanisa ni mama mwenye upendo na kwamba, Yesu Kristo amemwaga damu yake kwa ajili ya wote ili waweze kukombolewa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Kwa namna ya pekee, baba Mtakatifu analihamasisha Kanisa nchini Italia kujikita katika mchakato wa majadiliano sanjari na ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, ili kukuza upendo, umoja na mshikamano wa dhati bila ubaguzi. Kanisa lijitahidi kushirikiana na watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha, tamaduni, jumuiya na ujuzi ili kujenga jamii inayotegemeana na kushikamana bila kujali itikadi, mahali anapotoka mtu au dini au imani yake.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa wajenzi wa Italia kwa kuonesha mfano bora wa kuiga katika kuzungumza na kutenda; kwa kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya kisiasa na kijamii sanjari na kushuhudia imani katika matendo yanayojenga uhusiano mwema kati ya Mungu na jirani, tayari kuwa huru kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Kamwe wasioneshe ubaguzi katika maisha yao. Kanisa Katoliki nchini Italia liendelee kujipambanua kwa upendo na huduma kwa maskini; kwa kujenga na kudumisha umoja na udugu; kwa kulinda na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote sanjari na kuwa kweli ni chamchemi ya furaha hata kama kuna magumu yanayowaandama.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake kwa kuitaka Familia ya Mungu nchini Italia kujenga na kudumisha mwelekeo wa Kisinodi; kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha katika sera na mikakati yake ya kichungaji. Kanisa liendeleze kipaji cha ugunduzi kwa kutumia vyema utajiri na rasilimali iliyopo nchini Italia, ili kuharakisha ujenzi wa nchi yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.