2015-11-09 07:47:00

Umefika wakati kwa Kanisa Katoliki Italia kuadhimisha Sinodi ya Kitaifa!


Yesu Kristo ni kielelezo cha ubinadamu mpya ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Kongamano la tano ya Kikanisa Kitaifa nchini Italia linalofanyika Jimbo kuu la Firenze, kaskazini mwa Italia kuanzia tarehe 9 hadi 13 Novemba 2015. Ni kipindi cha siku tano ambacho kinawahusisha viongozi wakuu wa Kanisa nchini Italia ili kuweza kujadili changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha ya watu, tayari kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kama wanavyokazia Mababa wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican.

Huu ni mwaliko kwa Kanisa nchini Italia kuendelea kuwa karibu na watu kwa kusikiliza na kujibu kilio chao, tayari kuwatangazia Injili ya mapendo na matumaini kwa wale waliokata tamaa kutokana na changamoto mbali mbali za maisha. Hii ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda kwa kulifanya Kanisa kuwa kweli ni chombo cha huduma ya upendo na mshikamano kati ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anashiriki katika kongamano hili na anatarajiwa, Jumanne tarehe 10 Novemba 2015 kuzungumza na wajumbe.

Kongamano linajikita katika mazungumzo, shuhuda za maisha; majadiliano ya kiekumene na baadaye, kutoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Kongamano hili linatarajiwa kufungwa na Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Huu ni wakati wa kusali, kutafakari na kuibua vipaumbele vya Kanisa nchini Italia, tayari kuvifanyia kazi, lakini baada ya majadiliano ya kina na wadau mbali mbali. Pengine anasema Askofu Nunzio Galantino umefika wakati kwa Kanisa nchini Italia kuadhimisha Sinodi ya Kitaifa. Huu utakuwa ni wakati wa kujipyaisha katika masuala ya imani, maadili na utu wema; wakati wa kujadiliana na kuweka mikakati ya maisha ya kiroho na kijamii pamoja na kuwashirikisha wadau mbali mbali, ili kweli yale yanayoamriwa yatoke kwa waamini wenyewe kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili.

Hii ni kiu ya waamini kutaka kufanya hija ya pamoja katika maisha yao ya kila siku. Kongamano hili linawashirikisha wajumbe elfu mbili na mia tano kutoka sehemu mbali mbali za Italia. Lengo ni kujenga utamaduni kwa Kanisa kusikiliza zaidi na zaidi kilio cha watoto wake badala ya kufanya maamuzi yanayotolewa na viongozi wachache wa Kanisa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili, kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kutumia lugha inayofahamika na waamini wengi. Kristo waliyemtazama, awasaidie kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi wengi nchini Italia, kwa kujikita katika ubinadamu na utu mpya kwa kuachana na utu wa kale uliochakaa kama jani la mgomba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.