2015-11-09 11:42:00

Majadiliano yanayojikita katika sakafu ya mioyo ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na Kikundi cha watu wanne kutoka Tunisia, ambacho kimeshikiri kikamilifu katika mchakato wa majadiliano yaliyojikita katika mikono, lakini zaidi kutoka mioyoni mwao, leo hii Tunisia inaendelea kuandika historia tofauti kabisa katika misingi ya haki, amani na utulivu. Kikundi hiki kimeundwa na  Mohamed Fadhel Mahfoudh, Abdessatar Ben Moussa, Wided Bouchamaoui pamoja na Houcine Abbassi, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2015.

Baba Mtakatifu na wageni wake waliweza kuzungumza kwa takribani dakika kumi na tano na wao wamemshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwa kweli ni shuhuda na mjenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu amewazawadia wageni wake medali yake ya Kipapa pamoja na nakala ya Waraka juu ya utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, Laudato si. Wao pia wamemzawadia Baba Mtakatifu Picha ya Mahatma Gandhi, kiongozi aliyejipambanua kwa kutafuta suluhu katika migogoro ya kijamii kwa njia ya amani na majadiliano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.