2015-11-09 08:03:00

Mageuzi ndani ya Kanisa yanaletwa kwa njia ya sala na utakatifu wa maisha!


Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 8 Novemba 2015, Baba Mtakatifu Francisko alionesha masikitiko yake kutokana na wizi wa nyaraka za siri kutoka Vatican, jambo ambalo limeleta usumbufu mkubwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Amekaza kusema, wizi wa nyaraka za siri ni kitendo cha jinai ambacho kamwe hakiwezi kulisaidia Kanisa wala kumsaidia Yeye binafsi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mchakato wa kuleta mageuzi ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, nyaraka zote hizi, tayari zilikuwa zinafahamika kwake binafsi na kwa wasaidizi wake wa karibu na kwamba, tayari zilikuwa zimekwishafanyiwa kazi na matunda yake yanaanza kuonekana. Baba Mtakatifu anakaza kusema, vitendo hivi vya jinai vinavyosikitisha, kamwe havitamzuia wala kumkatisha tamaa yeye binafsi pamoja na wasaidizi wake wa karibu kuendelea na hamu ya kutaka kuleta mageuzi, kazi inayofanywa na kila mwamini kwa njia ya sala na utakatifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anawashukuru waamini wote na kuwaomba kuendelea kusali kwa ajili yake na Kanisa katika ujumla wake na kamwe wasihuzunishwe, bali waendelee kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, katika maadhimisho ya Siku ya Shukrani, inayoongozwa na kauli mbiu “Ardhi ni kwa ajili ya mafao ya wote”. Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni watawala wazuri wa rasilimali ardhi kwa kuwajibika, ili matunda yake yaweze kweli kuwanufaisha watu wote.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wakulima wanaotunza ardhi ili iweze kuzalisha chakula kwa wote kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho. Anaungana na waamini wa Jimbo kuu la Roma katika maadhimisho ya Siku ya kutunza mazingira, nyumba ya wote, tukio ambalo limeboreshwa kwa maandamano kwa ajili ya utunzaji bora wa mazingira!

Jumatatu tarehe 9 Novemba 2015 Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linaanza maadhimisho ya Kongamano la tano kitaifa, huko Jimbo kuu la Firenze, linalowashirikisha Maaskofu na wajumbe kutoka katika majimbo yote ya Kanisa Katoliki nchini Italia. Hili ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia, kwani ni kielelezo cha umoja na tafakari na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki tukio hili siku ya Jumanne, tarehe 10 Novemba 2014, akitokea Jimboni Prato. Mwishoni, amewakumbuka Wadominikani wanaoadhimisha Jubilei ya miaka mia nane tangu Shirika lao lilipoanzishwa. Amewashukuru na kuwapongeza kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.