2015-11-09 15:21:00

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani Jimbo kuu la Cracovia, Poland


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 9 Novemba 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Andrzej Duda wa Poland, ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamepongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Kanisa Katoliki na Serikali ya Poland, hususan mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wa Poland katika ujumla wao. Wamegusia kuhusu hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland, kunako mwaka 2016 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia.

Viongozi hawa wawili baadaye wamegusia masuala mbali mbali ya kikanda na kimataifa, kwa kujikita hasa katika umuhimu wa kukuza na kuendeleza tunu bora za maisha ya kifamilia; kuwahudumia na kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii bila kusahau kuonesha ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya maisha. Baadaye viongozi hawa wameangalia pia umuhimu wa kujenga na kudumisha amani na usalama; mgogoro wa kivita huko Ukraine pamoja na Mashariki ya Kati.

Rais Duda pamoja na ujumbe wake ambao, umekuwepo mjini Vatican, tangu Jumapili tarehe 8 Novemba ambako jioni hiyo wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II, lililoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.