2015-11-07 11:05:00

Wakristo onesheni mshikamano wa dhati ili kukabiliana na changamoto mamboleo


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja miongoni mwa Wakristo anasema kuna changamoto nyingi zinazowakabili Wakristo na zinapaswa kuwa ni kiungo cha umoja na mshikamano, ili kuweza kuzipatia ufumbuzi wa pamoja, kwa kuzingatia: haki msingi za binadamu, maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanuni maadili, changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo ni mambo ambayo yanaweza kushughulikiwa kwa pamoja na Wakristo wote.

Kardinali Koch ameyasema haya katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kufuatia Kongamano la kimataifa lililokuwa linafanyika huko Tirana, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ubaguzi, dhuluma, kifodini: Ufuasi wa Kristo kwa pamoja”. Ni mkutano ambao umewajumuisha viongozi wakuu wa Makanisa mia moja na arobaini kutoka katika Nchi sabini ulimwenguni. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wahusika, alionesha masikitiko yake makubwa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya dhuluma, nyanyaso na mauaji dhidi ya Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kardinali Koch anakaza kusema, kuna haja kwa Wakristo kuunganisha nguvu ili kujenga umoja na mshikamano wa dhati, tayari kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia.

Kanisa Katoliki hata kama si mwanachama wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC), lakini limeendelea kushirikiana na Makanisa mengine duniani kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili; sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani. Mkutano wa Tirana umesaidia kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo, ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Wakristo wanauwawa, wanadhulumumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Makanisa yanachomwa moto, alama na utambulisho wa kidini vinaharibiwa, zote hizi ni chuki dhidi ya Wakristo. Lakini, Makanisa pamoja na mambo yote haya, yanaendelea kuhamasishwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu pasi na kulipizana kisasi. Makanisa yaendelee kujielekeza katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama inavyojionesha kwa Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas, huko Mashariki ya Kati.

Huko Makanisa yanaendelea kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi; yanajikita katika mchakato wa maendeleo endelevu kiroho na kimwili; kwa kuwajengea wanawake uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha pamoja na kuwapatia vijana wa kizazi kipya elimu makini, ili kupambana vyema na mazingira, tayari kuleta mabadiliko katika jamii. Makanisa yako pia mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; lengo ni kutetea utu na heshima ya binadamu sanjari na ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kardinali Kurt Koch anakaza kusema, Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika wanaendelea kuhifadhiwa katika moyo wa Kanisa Katoliki. Jambo la msingi ni kwa Wakristo wote kuendelea kushikamana, ili kwa pamoja waweze kutoa majibu muafaka kwa changamoto mamboleo, ili kuendelea kumfuasa Kristo na kumtolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu wanaowazunguka. Hii ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga, ili watu wengi wapate kumwamini Kristo Yesu kuwa kweli ni Bwana na Mwalimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.