2015-11-07 10:32:00

Dr. Magufuli watumikie watanzania wote bila ubaguzi; dumisha utawala wa sheria


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anampongeza Rais Dr. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa, kuapishwa na hatimaye kuanza kuchapa kazi ya kuwatumikia watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vya, imani na mahali wanapotoka. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linamwomba, Rais Magufuli kutoa kipaumbele cha kwanza kwa masilahi ya kitaifa, ustawi na maendeleo ya watanzania wote. Dr. Magufuli atambue kwamba, kwa sasa ni Baba wa watanzania wote na kwamba, awasaidie watanzania kuwa tena na imani na Serikali yao kama kielelezo cha utekelezaji wa kiu ya mabadiliko iliyooneshwa na watanzania wengi wakati wa kampeni na hatimaye uchaguzi mkuu uliohitimishwa hivi karibuni! Awatumikie watanzania wote, ili waweze kusonga mbele katika mchakato wa kujipatia maisha bora zaidi.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha amemwomba Rais Magufuli kuonesha uzalendo, usawa, upendo na mshikamano wa kitaifa, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mustakabali wa taifa badala ya kuangalia pengine masilahi ya Chama cha Mapinduzi. Askofu mkuu Lebulu anakaza kusema, ni vyema ikiwa kama Dr. Magufuli atajitahidi kumuiga Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote, leo hii anakumbukwa na wengi ndani na nje ya Tanzania.

Askofu mkuu Lebulu anasema, Tanzania kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya kura ya maoni kuhusu Katiba inayopendekezwa, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, maoni yaliyotolewa na watanzania wengi na kufanyiwa kazi na Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba yanaheshimiwa na kamwe yasitupwe jalalani kana kwamba si mali kitu!

Naye Askofu Severine NiweMugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara anasema, Tanzania kwa sasa inaendelea kuganga na kuponya madonda ya kinzani na upinzani uliojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu. Ni matumaini yake kwamba, Dr. Magufuli atatekeleza kwa dhati ahadi ambazo alizitoa wakati akigombea Urais, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unazingatiwa na wote. Viongozi wa Serikali wawe wa kwanza kuonesha mfano wa utawala bora kwa kujikita katika sheria za nchi pamoja na kuwatendea watanzania wote haki bila ya kujali itikadi zao, imani, makabila wala anakotoka mtu!

Rais John Pombe Magufuli kwa upande wake anaendelea kukazia: uadilifu, bidii, uaminifu na kujituma bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi. Umefika wakati kwa wafanyakazi Serikalini kuacha kufanya kazi kwa uzembe na mazoea. Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini Tanzania limepiga rufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya kisiasa kwa madai ya kuwepo kwa mihemuko ya kisiasa inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu nchini Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.