2015-11-05 07:43:00

Utawala bora, ukweli na uwazi ni mambo msingi yanayotekelezwa Vatican!


Vatican inaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi na utawala bora. Uchapishaji wa vitabu viwili ambavyo ni matokeo ya uvujishaji wa nyaraka za siri kutoka Vatican ni kitendo cha jinai. Vitabu hivi kimsingi vinazungumzia kuhusu masuala ya uongozi, fedha na uchumi wa Vatican. Watu waliohusika kuvujisha nyaraka za siri watashughulikiwa kadiri ya sheria za Vatican.

Hii ni tafakari inayotolewa na Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican kuhusisna na kashfa ya kuvujisha nyaraka za siri kutoka Vatican ambayo kwa sasa watu wawili wanashikiliwa na Polisi na kwamba, hakuna tena mtu mwingine anayehusishwa na kashfa hii. Sehemu kubwa ya mambo yaliyoandikwa vitabuni humo ni yale yaliyokwishajadiliwa na hatimaye yakatolewa maamuzi. Takwimu zilizomo kwenye vitabu hivi ni zile zilizokusanywa kutokana na maamuzi ya Baba Mtakatifu Francisko, ili kusaidia Tume ya COSEA kufanya upembuzi yakinifu, tayari kuanza mchakato wa mageuzi makubwa katika masuala ya fedha, uchumi na uongozi wa Vatican katika ujumla wake.

Padre Lombardi anasema, nyaraka nyingi zinazofanyiwa rejea kwenye vitavu hivi ni zile ambazo zimechotwa kutoka kwenye masjala ya COSEA iliyoundwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 na kuvunjwa baada ya kumaliza kazi zake. Kumbe, hizi si nyaraka ambazo zilikuwa zinakwenda kinyume cha utashi wa Baba Mtakatifu Francisko wala viongozi wandamizi kutoka Vatican. Kuhusu Mfuko wa Akiba ya Uzeeni kutoka Vatican unaodaiwa kwamba, unaonekana kufilisika, si kweli kwani taarifa na takwimu zilizotolewa na wahusika zinazonesha kwamba, hali ni nzuri na inatia moyo!

Padre Lombardi anakaza kusema, rasilimali inayomilikiwa na Vatican inalenga kwa namna ya pekee kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuliongoza Kanisa la Kristo. Rasilimali hii inaweza kuwa inaratibiwa na vyombo vya Vatican sehemu mbali mbali za dunia. Vyanzo vya rasilimali hii ni vingi na kwamba, ni matunda ya historia na mikataba iliyowekwa kati ya Vatican na wahusika, kama ilivyo kwa nchi ya Italia. Rasilimali fedha ni kwa ajili ya kulisaidia Kanisa katika utekelezaji wa dhamana yake ukarimu kwa maskini pamoja na kuendeleza huduma zinazotolewa na wawakilishi wa Vatican 180 waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia. Rasilimali fedha inachangia pia ustawi na maendeleo ya Makanisa mahalia. Mfuko wa Mtakatifu Petro unatekeleza majukumu haya.

Umefika wakati anasisitiza Padre Lombardi kujikita katika misingi ya haki, sheria, kanuni na taratibu, ili kuweza kusahihisha, kurekebisha pamoja na kuondoa wasi wasi pale unapojitokeza, ili utawala wa sheria uweze kushika mkondo wake badala ya kila wakati baadhi ya waandishi wa habari kujitumbukiza katika uvunjaji wa sheria na kanuni maadili ya kazi zao. Tume ya COSEA ilikwishahitimisha kazi yake, lakini ushauri uliotolewa unaendelea kufanyiwa kazi na baadhi ya matunda ya ushauri huu yanaonekana kwa sasa. Hii ni pamoja na kuundwa kwa Sekretarieti ya uchumi mjini Vatican inayoshughulikia masuala ya fedha na uchumi.

Kumbe, taarifa ya nyaraka zilizovujishwa tayari zilikwishafanyiwa kazi na kwamba, vitabu hivi ni kama “debe tupu ambalo haliachi kutika”, vinaonesha hali ya mtunzi kuchanganyikiwa na kukosa ukomavu katika ukweli na uwazi, kutokana na kujikita katika masuala binafasi anayoyafahamu mwenyewe! Mchakato wa utekelezaji wa utawala bora mjini Vatican unaendelea pasi na kigugumizi wala makunyanzi. Hii ni dhamana inayotekelezwa na Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu, wanatambua changamoto, kinzani na fursa zilizopo.

Viongozi wa Kanisa wataendelea kutumia rasilimali iliyopo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa: kiroho na kimwili. Jambo la msingi ni kuendelea kukazia umuhimu wa kujikita katika ukweli na uwazi pamoja na kuzima kiu ya familia ya Mungu katika ujumla wake. Utawala bora unaojikita katika ukweli na uwazi ni kati ya mambo msingi yanayoendelea kufanyiwa kazi na Vatican na kwamba, kuna wafanyakazi wa Vatican wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo pasi na kujibakiza.

Padre Lombardi anahitimisha tafakari yake ya kina kuhusu kashfa iliyojitokeza hivi karibuni mjini Vatican kwa kusema kwamba uchunguzi unaendelea kufanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusiana na Bwana Gianpietro Nattino anayeshutumiwa kuchukua kiasi kikubwa cha fedha kutoka Benki ya Vatican na kukihamishia nchini Uswiss.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.