2015-11-05 10:30:00

Majadiliano ya kidini, haki na amani muhimu kwa ustawi wa wengi Afrika ya kati


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 30 Novemba 2015, huko Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, anatarajiwa kupandikiza mbegu ya matumaini mapya, hususan Familia ya Mungu nchini Afrika ya Kati, ambako wananchi wanaendelea kuteseka kutokana vita. Baba Mtakatifu ameguswa na mahangaiko na mateso ya wananchi hawa anawataka sasa kuanza mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana kwa kujikita katika umoja na upatanisho wa kitaifa, haki na amani.

Ni watu ambao kwa muda mrefu wamekosa matumaini anasema Padre Hermann Tanguy Pounekrozou kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ambaye kwa miaka mingi amekuwa akishirikiana na Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji. Wananchi walitarajia kufanya uchaguzi mkuu hapo tarehe 18 Oktoba, 2015, lakini Serikali haikuwa na uwezo wa kuwahakikishia wananchi wake usalama na amani wakati wa mchakato mzima wa zoezi la upigaji kura na hivyo uchaguzi hakufanyika kama ilivyotarajiwa!

Kimsingi watu wanataka kuona mabadiliko chanya, lakini kwa bahati mbaya, kampeni za uchaguzi zimegubikwa na vitendo vya rushwa na ufisadi. Baadhi ya viongozi wanaowania madaraka walikuwa wanaunga mkono mapinduzi ya Serikali yaliyofanywa na Kikundi cha Seleka, kunako mwaka 2013. Bangui bado ni mji ambao umesheheni vitendo vya wizi na uporaji; ujambazi na utekaji nyara ni mambo ya kawaida. Bado Seleka na Balaka vinapimana nguvu, kwa kuendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Padre Hermann anasema kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyobandikwa picha ya udini, majadiliano ya kidini pia yamekuwa yakisuasua. Baadhi ya watu wanadhani kwamba, hii ni vita ya kidini, lakini ukweli wa mambo ni vita inayojikita katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, kwa baadhi ya viongozi kuwa na uchu wa mali na madaraka, kiasi cha kukumbatia utamaduni wa kifo.

Serikali iliwanyanyasa na kuwadhulumu wafanyabiashara, ambao wengi wao ni waamini wa dini ya Kiislam na matokeo yake, Seleka ikatumia mwanya huu kujitafutia umaarufu kwa kuonesha kwamba, hii ilikuwa ni vita ya kidini, ili kuwapatia waamini wa dini ya Kiislam ukombozi wa kweli. Kumbe, kinyume chake ni watu waliokuwa na uchu wa mali na madaraka walitaka kutumia udhaifu wa Serikali kwa mafao yao binafsi, hatari kubwa katika mafungamano ya kijamii! Wakristo kwa upande wao, wakiwa wamejifunika katika mwamvuli wa Balaka, wanawatuhumu waamini wa dini ya Kiislam kwa kushirikiana na Seleka kuipindua Serikali kutoka madarakani.

Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Afrika ya kati amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam kwa kujikita katika uhalisia wa maisha, ili wananchi waweze kuishi katika hali ya amani na utulivu na kwamba, tofauti zao za kidini ni utajiri na urithi mkubwa kwa wananchi wa Afrika ya kati. Juhudi za majadiliano ya kidini zinaungwa mkono pia na Imam Omar Kobine Layama. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo itaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.