2015-11-05 10:58:00

Huduma ya upendo kwa maskini ni changamoto endelevu Ufilippini!


Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila, Ufilippini, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya kufunga Mwaka wa Maskini, ulioitishwa na kuzinduliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini mwanzo mwa mwaka 2015. Jimbo kuu la Manila litafunga Mwaka wa Maskini hapo tarehe 7 Novemba 2015, tayari kwa waamini kuendeleza ari na mwamko walioupata katika maadhimisho ya Mwaka wa Maskini, ili kuwasaidia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Askofu Tagle ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anakaza kusema, Kanisa halina budi kujitambulisha na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, huduma kwa maskini ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa, kwani maskini ndio kiini cha Habari Njema ya Wokovu, wanaopaswa kuonjeshwa matumaini.

 

Hii ni changamoto ambayo inatolewa pia na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasaidia maskini wa kiroho na kimwili katika mahitaji yao msingi pamoja na kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya mwanadamu. Ni mwaliko wa kupambana na mambo yote yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini wa hali na kipato! Maskini wanapaswa kwanza kabisa kuheshimiwa na kuthaminiwa kabla ya mambo mengine yote!

Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 25% ya wananchi wa Ufilippini wanaishi katika kiwango kikubwa cha umaskini wa hali na kipato. Hawa ndiyo wanapaswa kujengewa uwezo kwa kupewa elimu makini; kupatiwa fursa za ajira na kushirikishwa kikamilifu katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo endelevu. Hii ni changamoto makini ya kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote, kwani wananchi wengi wa Ufilippini ni waathirika wakubwa wa majanga asilia pamoja na ukosefu wa haki msingi za kibinadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linawaalika waamini kusimama na kutoka kimasomaso, ili kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya wakati huu Kanisa nchini humo, linapomshukuru Mungu kwa maadhimisho ya Jubilei ya miaka mia tano ya uwepo na ushuhuda endelevu wa Kanisa Katoliki katika maisha ya watu. Tangu mwaka 2013 hadi mwaka 2021, waamini wanaendelea kuadhimisha Mwaka huu kwa kuangalia pia dhamana na nafasi ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa; umaskini pamoja na familia. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maandalizi ya Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu kimataifa litakaloadhimishwa Jimbo kuu la Cebu, Ufilippini kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 31 Januari 2016. Waamini watapata nafasi ya kupembua kuhusu Familia na Ekaristi Takatifu, tema tete iliyofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi ya familia iliyohitimishwa hivi karubuni mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.