2015-11-05 09:13:00

Acha mkono wa birika, ili Injili iwaguse wengi!


Kuna maangalisho yenye lengo la kukuepusha na hatari kama vile: “Angalia utelezi, Angalia kona kali! Tahadhari mbwa mkali! Tahadhari waya wa umeme!” Ukimwi unauwa! Jikinge na Ebola! Usipige picha! Maangalisho mengine ni ya ushauri mwema, kama vile:"Akili ni nywele kila mtu ana zake! "Kila zama na kitabu chake"! “Tumia vizuri mali yako, Fikiri kabla ya kunena, Tunza siri! Leo kwa njia ya picha mbili za wanaume na wanawake tunaalikwa kutafakari maangalisho na ushauri muhimu tunaopaswa kuzingatia katika maisha.

Picha ya kwanza ya tahadhari ya kutoiga mfano mbaya inatoka kwa wanaume. Yesu anawatahadharisha wafuasi wake kwa ukali dhidi ya Waandishi. Historia na mchango wao katika jamii na taifa la Wayahudi ni ndefu kidogo. Watu wa Mashariki walikuwa na utamaduni wa kuhifadhi maandishi na sheria za Wafalme wao kama vile Farao wa Misri na Hamurabi wa Babiloni. Wayahudi walipokuwa utumwani Babiloni walianza kuandika kitabu cha Sheria za Musa kiitwacho Torah. Kwa hiyo Waandishi hao wa Tora wakaja pia kuwa wafasiri rasmi wa Tora na Maandiko katika  mahakama na mahekaluni  – Maelezo ya ufasiri wa Tora yapo katika Yoshua bin Sira 13 –.

Yesu aliutambua pia mchango wa Waandishi, lakini kipengee kilichomkera na kumtia hasira ni tabia ya Waandishi ya kutaka kuheshimiwa kama miungu, kisha tabia ya unafiki na ile ya kuwanyonya maskini hasa wajane. Yesu anawatahadhaliwa wafuasi wake kwa ukali kujiangalia sana na tabia hiyo: “Jihadharini!” kwa Kigiriki ni blepete ni amri – Daima waangalie, waepuke! Jihadharini nao! Waogopeni! Muwe macho nao! – Kisha anaonesha waziwazi alama zinazowatambulisha Waandishi hao:

Mosi, “wanapenda kutembea wamevaa mavazi marefu.” Hayo ni mavazi ya pekee yanayowatofautisha na watu wengine. Alama ya pili ni “Kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu,” yaani kupenda heshima ya pekee anayostahili kupewa Mungu peke yake. Yesu anawataka  wanafunzi wake wawe watu kawaida wa utumishi kwa upendo. Alama ya tatu ni kuwa “Hula nyumba za wajane.” Hawa wajane walikuwa maskini na wanyonge walikuwa wanaishi kwa kudra ya Mungu. Waandishi walikuwa wanawanyonya kwa kupokea ufadhili toka kwao. Alama ya nne, “kwa unafiki husali sala ndefu.” Huo ni unafiki mbele ya Mungu mwenyewe, kwa kusali sala refu halafu unadhulumu maskini. Yesu kwa mara ya kwanza anatamka hukumu kwa watu aina hiyo kwamba “hao watapata hukumu iliyo kubwa.”

Baada ya kuonesha vigezo vibovu vya kuwatambua Waandishi, Yesu anatupatia picha ya pili  ya alama na vigezo vya maisha mazuri tunayoweza kujifunza toka kwa mwanamke. Yesu alikuwa amesimama Hekaluni karibu na masanduku kumi na matatu ya kutolea sadaka yenye kuandikwa kila moja nia ya sadaka. Kila aliyetaka kutia sadaka yake, aliionesha kwanza kwa kuhani. Kama sadaka ilikuwa nono kuhani aliweza pia kumshukuru na kumpongeza mtoaji. Katika kisanduku cha kumi na tatu kisichoandikwa nia ya sadaka, humo kila mmoja aliweza kutia sadaka kiasi alichonacho tena kwa siri bila kuonekana. Yesu alimwona mjane mmoja anatia vijisenti vyake viwili vya thamani ya nusu pesa katika kisanduku hicho.

Kwa kawaida “vijisenti” hivi vilitumika hekaluni tu kwa kutolea sadaka kwani kwa matumizi ya biashara ilikuwa inatumika pesa ya Mrumi. Yesu akasema: “Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina.” Kwa hiyo mjane huyu ni mfano wa mfuasi wa kweli asiyetaka kuonekana na yeyote yule anapofanya tendo la huruma na la upendo wote. Kisha Yesu anatoa maelezo: “hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyo navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Kwa Kigiriki Hebalen, olon ton bion autes yaani, alitia maisha yake yote. Kwa hiyo ili kuwa mfuasi wa kweli wa Yesu, yabidi kuwa kama mjane huyu maskini. Mfuasi wa kweli sio kama wale waandishi wanaojionesha wanapofanya tendo jema, bali ni kama huyu mjane maskini asiyejionesha na maisha yote yanakuwa zawadi ya Mungu kwa ajili ndugu.

Katika Injili nzima ya Marko kuna wanawake kadhaa walio mfano bora wa kufuata kinyume cha wanaume. Mwanamke wa kwanza ni mkwe wa Petro aliyekuwa amelala kitandani hawezi homa. Yesu akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia. (Mk. 1:29-31). Mwanamke huyu anayetumikia ni mfano kwetu wa upendo. Mwanamke wa pili  ni yule wa kutoka damu miaka kumi na miwili. Baada ya kugusa vazi la Yesu alipona msiba wake. Yesu anamwambia “Binti imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.” (Mk 5:25-34) Mwanamke huyu ni mfano wa imani kwa vile alikuwa anapoteza polepole uzima wake – kwani damu ni alama ya uzima – sasa amerudishiwa tena maisha yake kwa kugusa vazi la Yesu.

Mwanamke anatufundisha kugusa Injili (Habari njema) kwa imani yaani, kufuata mapendekezo ya Injili kwa imani. Mwanamke wa tatu ni Msirofoinike. Kutokana na imani yake akamshangaza hata Yesu aliyemwambia: “Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako; pepo amemtoka binti yako.” (Mk. 7:24-29) Mwanamke wa nne ni huyu mjane maskini leo. (Mk 12:41-44). Mwanamke wa tano ni yule anayemmiminia Yesu marashi ya bei mbaya kule Bethania ikiwa ni alama ya kupenda sana bila kipimo.

Katika wanawake hawa watano tunapata mifano bora ya imani na upendo anaopaswa kuigwa na mfuasi wa Kristo. Laiti kama waamini na viongozi wa dini wanaovaa misalaba na nguo nzuri za ibada, wanaokaa katika nyumba za ibada, wanaosali vizuri, wangekuwa kama wanawake hawa wenye imani kuu na upendo usio na mwisho wenye kujiaminisha kwa Mungu katika imani na kufadhili kwa upendo, hapo Injili ingekuwa kweli ni Habari Njema ya furaha na wokovu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.