2015-11-04 11:59:00

Wakenya shikamaneni katika umoja, upendo na udugu!


Simameni imara katika imani, msiogope! Ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Kenya kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 27 Novemba 2015. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaendelea kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati, ili kumwezesha Baba Mtakatifu Francisko kukoleza umoja na mshikamano wa kitaifa ambao kwa miaka ya hivi karibuni umetikiswa sana kutokana na misimamo mikali ya kidini, ukabila na umajimbo, mambo yanayokuzwa na kudumishwa na wanasiasa kwa ajili ya masilahi yao.

Askofu Afred Rotich anasema, kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Kenya kutokana na mitafaruku ya kisiasa. Wananchi wa Kenya wanapaswa kushinda kishawishi cha ukabila ili kuambata umoja wa kitaifa, tayari kuunganisha nguvu zao katika mapambano dhidi ya umaskini, ukosefu wa ajira na hali ngumu ya maisha. Misigano ya kisiasa kati ya viongozi wa kisiasa ni hatari kwa mafungamano ya kijamii nchini Kenya. Hii ni changamoto kwa viongozi wa kisiasa kujenga utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana katika ukweli na uwazi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati ili kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko anapotembelea nchini mwao kama mjenzi wa daraja la upatanisho, haki na amani. Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza bila kusahau utu na heshima ya binadamu. Parokia zinahamasishwa kuhakikisha kwamba, walau zinapeleka mahujaji kwenye Ibada ya Misa Takatifu inayotarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu hapo tarehe 26 Novemba 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.