Baba Mtakatifu anasema, kama ndani ya familia, tutajifunza kuomba samahani na kuheshimiana mmoja kwa mwingine, kuifunga siku kwa kuomba msamaha bila kuchelewa, tutaweza jenga familia thabiti zaidi na hata kupunguza ukatili ndani ya jamii.
Papa ametoa rai hiyo wakati wa Katekesi yake kwa mahujaji na wageni kama mwendelezo wa majadiliano , kufuatia kukamilika kwa Sinodi ya Maaskofu iliyotafakari umuhimu wa Familia katika utume wa kanisa na jamii kwa ujumla. Hata hivyo alionya kwamba maelezo yake si kwamba yanatoa maamuzi yake ya mwisho juu ya majadiliano ya Sinodi ya familia, bado muda wa kufanya hivyo , maana anahitaji muda zaidi ya kutafakari yaliyojadiliwa. Lakini bado ni muhimu kuzungumzia mada hii ya familia, kutokana na umuhimu wake kwamba, ndani yake kuna kujifunza mengi , kama pia shule ya kwanza, ya kujifunza maisha na thamani ya kuomba msamaha. Maelezo ya Papa yalilenga katika maneno ya sala ya Baba yetu, ambamo waamini kila siku huomba kusamehewa kwa yale waliyokosea na pia huomba neema ya kusamehe wengine.
Papa alionyesha kutambua jinsi ilivyo vigumu kusamehe , lakini akasema ni hitaji muhimu katika ukomavu wa mtu binafsi na katika uwezo wa kutambua na kukiri makosa yetu na kufanya marekebisho katika mahusiano yaliyo vunjika au kulegalega. Tendo la kuomba msamaha, huanzia ndani ya familia. Na kwamba msamaha ni kiungo chenye kuongeza upendo ulio imara zaidi kati ya wanafamilia, katika kutembea pamoja kwenye njia yao ya maisha. Na hufanya jamii kwa ujumla, kuwa na upendo zaidi na ubinadamu zaidi. Papa anaitaja familia kuwa ni jiwe kuu la msingi katika kujenga maisha yetu na ishara fasaha katika utambulisho wa kuwa mfuasi wa Kikristo na katika kutii mapenzi ya Baba wa Mbunguni .
Papa aliendelea kusema, ni lazima kuwa na utambuzi kwamba , maisha hayasimami na hasa maisha ya familia yanaendelea kusonga mbele, kamwe hayasimami. Hvyo familia daima ziko safarini , zikiendelea kuandika kurasa na kurasa za uzuri wa maisha ya kiinjili kwa familia. Na hasa katika dunia ambayo wakati mwingine inakuwa na ukame wa maisha na upendo , inapaswa kila siku kuzungumzia juu ya zawadi hii kubwa ya ndoa na familia.
Katika mafundisho haya , Papa amesisitiza msamaha , kusamehe na kuheshimiana mmoja kwa mwingine, kuwa ni nguzo kuu ya maisha yenye ya furaha , yenye kuwa na upendo wa dhati, kama zawadi ya thamani yenye kuidumisha familia, kwa majitoleo ya sadaka binafsi kwa ajili ya wengine. Amesema bila uwepo wa kusamehe, na bila upendo, familia kama hiyo husambaratika mara. Papa alieleza na kurejea mara kwa mara juu ya sala ya Baba Yetu, iliyofundishwa na Yesu mwenyewe. “Utusamehe makosa yetu, kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea, na pia Yesu alisema: "Mkiwasamehe watu wengine makosa yao, Baba yenu aliye mbinguni pia atawasamehe ninyi (Mathayo 6,12.14-15). Na hivyo , Papa akaonya , haiwezekani kuishi bila kusamehe, na hasa uwepo wa maisha mazuri ndani ya familia, kwa kuzingatia kwamba, makosa kwa mara nyingi hutokana na udhaifu wetu wa kibinadamu, ikihamasishwa na ubinafsi wetu. Na hivyo kumbe kile kinachohitajika kwa kila mmoja, ni kuona umuhimu wa kuponya majeraha yanayoumiza. Haifai kuuguza kidonda kwa muda mrefu bila kukipatia dawa, maana kwa kadri kinavyokaa bila dawa ndivyo huzidi kuchimbika. Kumbe ni kufanya hima kuponya madonda hayo. Ni hitaji la kuomba msamaha na kuomba mapatano iwe kati ya mume na mke, au kati ya wazazi na watoto,, au kaka na dada, mkwe na mama mkwe n.k .
Baba Mtakatifu akitoa Katekesi hii kwa lugha ya Kiitalino alionyesha imani yake kwamba, familia zina uwezo wa kutembea pamoja katika njia ya Heri zilizo fundishwa na Yesu. Kujifunza na kufundisha jinsi ya kuomba msamaha au kusamehe mara moja, kwa kuheshimiana, kwa ajili ya uponyaji wa majeraha yanayoweza kujitokeza katika safari ya ndoa na familia. Na hivyo msamaha na kuheshimiana vinakuwa shina imara la maisha mazuri yaliyo imara zaidi yenye kupokelewa kama zawadi kati ya wanafamilia. Papa alieleza huku akionyesha imani yake kwamba, kwa hakika familia za Kikristo leo hii , zinaweza fanya mengi na pia kwa ajili ya Kanisa. Kwa maoni hayo, Papa alionyesha hamu yake kwamba katika Jubilee ya Huruma ya mungu , familia zitaweza gundua upya nguvu za msamaha, na kuiwezesha familia kubwa ya Kanisa kutangaza nguvu za upatanisho na upendo wa Mungu, ili pasiwe na mtu anayesahaulika katika msamaha huu katika maisha yetu ya kila siku.
All the contents on this site are copyrighted ©. |