2015-11-04 14:21:00

Novemba ni mwezi wa utunzaji bora wa mazingira!


Muungano wa Mashirika ya kitume ya Kanisa Katoliki Duniani, ulioanzishwa kunako mwaka 2015 kwa kuvijumuisha vyama vya kitume zaidi ya 230 kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi Cop21, utakaofanyika mjini Paris, Ufaransa mwezi Desemba 2015, umetenga mwezi Novemba kuwa ni mwezi wa utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Laudato si!

Lengo ni kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujipanga vyema zaidi ili kuweza kudhibiti sanjari na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utafunguliwa rasmi mjini Paris tarehe 30 Novemba na kufungwa rasmi hapo tarehe 11 Desemba 2015. Muungano huu ni sehemu ya utekelezaji wa changamoto iliyotolewa na  viongozi mbali mbali wa Kanisa kwa ajili ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa.

Viongozi wa Kanisa wanakaza kusema, makubaliano ya kimataifa yatakayofikiwa huko Ufaransa yajikite katika usawa, sheria na yanayotekelezeka ili kweli Jumuiya ya Kimataifa iweze kuonesha mageuzi makubwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza maelfu ya watu katika lindi la umaskini na magonjwa. Jumuiya ya Kimataifa iwahamasishe watu kuwa na mtindo wa maisha unaojikita katika mshikamano unaongozwa na kanuni ya auni; haki na upendo, kwa kushirikishana rasilimali ya dunia na changamoto zake, kwani mazingira, kimsingi ni nyumba ya wote na hifadhi ya zawadi ya maisha.

Viongozi wa Umoja wa Mashirika ya kitume ya Kanisa Katoliki Duniani yanaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuridhia sera na mikakati inayopania kudhibiti ongezeko la nyuzi joto duniani, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa watu wengi duniani. Taarifa ya Umoja huu, itawasilishwa kwa viongozi wa Serikali ya Ufaransa ambao ni mwenyeji wa mkutano huu, hapo tarehe 28 Novemba 2015 wakati wa mkutano wa dini na madhehebu mbali mbali kuhusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.