2015-11-03 11:41:00

Kumbu kumbu ya Miaka 20 ya Waraka wa Injili ya uhai na changamoto zake!


Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wake wa kitume Injili ya Uhai, Evangelium vitae, inayojikita katika mafundisho makuu ya Kanisa kuhusu umuhimu wa kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba,  kifo laini pamoja na hukumu ya kifo. Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho kimeshuhudia maendeleo makubwa katika sayansi ya tiba ya mwanadamu. Kunako mwaka 1995, Mtakatifu Yohane Paulo II akaibuka ili kutangaza Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Waraka huu wa kitume umekumbukwa kwa namna ya pekee kwa njia ya kongamano lililoandaliwa na Chuo kikuu cha LUMSA, kilichoko hapa mjini Roma na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka ndani ya Kanisa na watu mashuhuri waliochangia mawazo yao kuhusu umuhimu wa kushuhudia Injili ya uhai ambayo kwa sasa inatishiwa kwa kiasi kikubwa na utamaduni wa kifo.

Askofu Ignacio Carrasco de Paula, Rais wa Taasisi ya kipapa kuhusu maisha katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Waraka wa Injili ya Uhai ni muhimu sana na ni msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa kipaumbele cha kwanza kwa uhai wa binadamu, utu na mafao ya wengi. Kamwe binadamu hawezi kugeuzwa kuwa ni kichokoo cha tafiti za kisayansi na kwamba, kashfa ya utoaji mimba inaendelea kushika kasi ya ajabu hata wakati huu kama kilivyo pia kwa kifo laini.

Miaka ishirini iliyopita kifo laini au Eutanasia kama kinavyojulikana na wengi, halikuwa ni tatizo kubwa sana, lakini Mtakatifu Yohane Paulo II alikwishaona kuwa ni tishio kubwa kwa Injili ya uhai, ndiyo maana akawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Uhai. Askofu De Paula anakaza kusema, uhai wa binadamu si jambo la mtu binafsi wala uhuru wa mtu binafsi kwa sababu hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambayo mwanadamu amekabidhiwa kuilinda, kuitunza na kuidumisha.

Wakati huo huo, Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI anasema, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai; kazi kama kielelezo cha utimilifu na maisha ya binadamu na kwamba, siasa daima ilenge mafao ya wengi na wala si mtaji wa watu kutajirika. Waamini na wananchi wa Roma wanahitaji kuwa na viongozi bora watakaowasaidia kuadhimisha kikamilifu Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Kanisa litaendelea kujikita katika Mafundisho yake ya kutunza na kudumisha Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na utamaduni wa mwenye nguvu mpishe kwa kuwalinda wangonge na maskini katika jamii. Maisha, utu na heshima ya binadamu ni mambo matakatifu yanayopaswa kuheshimiwa na wote pasi na mjadala! Kanisa wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Familia limekaza kusema, linathamini sana maisha ya ndoa na familia na kwamba, hapa hakuna mbadala! Ndoa za watu wa jinsia moja ni kinyume cha mpango wa Mungu kwa mwanadamu na ukiukwaji wa kanuni maadili. Ndoa ya Kikristo inajengwa katika msingi wa upendo kati ya bwana na bibi na matunda ya muungano huu ni watoto ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Familia ni kiini cha jamii; maisha na utume wa Kanisa. Familia ni hazina ya binadamu na kamwe haina mbadala anakaza kusema Kardinali Angelo Bagnasco.

Kwa upande wake Teodora Rossi kutoka Chuo kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, Angelicum anapenda kuonesha uhusiano uliopo kati ya Injili ya uhai na Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote, Laudato si unaojikita katika ekolojia ya binadamu, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Binadamu anayo dhamana kubwa ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.