2015-11-03 10:55:00

Dini, haki na amani ni chanda na pete, kamwe havipaswi kusigana wala kukinzana


Viongozi wa kidini wanayo changamoto kubwa  ya kuhakikisha kwamba, wanasaidia mchakato wa kuleta mageuzi katika maisha ya watu ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano unaojikita katika majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, badala ya kuendekeza utamaduni uliopitwa na wakati kwa waamini kudhaniana vibaya na kutoheshimiana. Kuna haja ya kuendelea kushikamana kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi, haki na amani pamoja na kutafuta suluhu ya migogoro mbali mbali kwa njia ya majadiliano. Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Jean Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika ujumbe aliowaandikia wajumbe kutoka Barani Ulaya waliokuwa wanashiriki katika mkutano uliokuwa unapembua dhana ya amani.

Mkutano huu umewashirikisha wajumbe kutoka dini mbali mbali duniani na ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha tamko kuhusu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali kama njia ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano kati ya watu wa mataifa. Mkutano huu umeadhimishwa huko Castel Gandolfo, kuanzia tarehe 28 Oktoba hadi tarehe Mosi, Novemba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kuwaonesha wengine ukarimu bila woga ili kuwajengea imani. Wajumbe hawa pamoja na mambo mengine, wamejadili kuhusu utandawazi, woga unaojengwa dhidi ya waamini wa dini ya Kiislam, ubinafsi wa kutupwa.Anakaza kusema, Kanisa Katoliki linaendelea kuwahamasisha waamini wa dini mbali mbali duniani kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kardinali Tauran anakaza kusema, majadiliano ya kidini Barani Ulaya yanakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwa ni pamoja na woga wa kupoteza utambulisho wa kidini, hali inayopelekea uwepo wa misimamo mikali ya kidini kama njia ya kujihami; ukosefu wa maridhiano kati ya watu; dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutokana na vita pamoja na mipasuko ya kijamii pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wajumbe wamehamasishwa kutafuta njia zitakazoweza kuleta mageuzi katika maisha ya watu kwa kuwajengea imani na matumaini; haki, heshima na urafiki; umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali kwa ajili ya mafao ya wengi. Waamini wanakumbushwa kwamba, amani na dini ni sawa na chanda na pete na kwamba, utamaduni wa ubaguzi kwa misingi ya kidini ni hatari kwa mafungamano ya kijamii, hali inayoweza kusababisha kinzani, vita na mitafaruku ya kijamii. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kukemewa na viongozi wa kidini pamoja na wapenda amani wote.

Viongozi wa kidini wawe mstari wa mbele kushuhudia umoja na mshikamano unaobubujika kutoka katika sala, ibada na matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wahakikishe kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na wajenzi wa haki na amani na  kamwe si chanzo cha fujo, chuki na uhasama kati ya jamii. Majadiliano na ushirikiano ni kati ya utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho ambao waamini wanaweza kumegeana na kushirikishana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi katika umoja na utofauti; katika kweli na amani anasema Kardinali Jean Louis Tauran.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.