2015-11-03 08:27:00

Baba Mtakatifu Francisko kufungua lango la Jubilei ya huruma ya Mungu, Bangui!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican amegusia kuhusu umuhimu wa Sinodi ya familia iliyohitishwa hivi karibuni, mchakato wa Vatican kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia na China pamoja na hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika ambako anatarajiwa kutembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 30 Novemba 2015.

Kardinali Parolin anasema, baada ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia kusali, kutafakari na kushirikishana ujuzi, uzoefu na mang’amuzi yao ya shughuli za kichungaji kuhusiana na utume wa familia, wamemkabidhi Baba Mtakatifu Francisko hati elekezi kama sehemu ya mapendekezo yao kwa Kanisa katika kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Baba Mtakatifu kwa wakati wake, kwa kuzingatia mahitaji na changamoto zinazoendelea kuzikabili familia atatoa  maamuzi yake ni nini kiweze kufanyika.

Kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko ameruhusu hati elekezi inayobeba mapendekezo ya Mababa wa Sinodi ichapishwe na waamini waendelee kuyatafakari mapendekezo haya, huku wakiendelea kusubiri tamko jingine kutoka kwa Baba Mtakatifu mwenyewe. Kwa sasa waamini wengi wanasubiri kusikia yale yatakayotolewa na Baba Mtakatifu ili kukabiliana na changamoto, fursa na kinzani zinazojitokeza katika mchakato wa kuishi, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo ndiyo kauli iliyoongoza maadhimisho ya Sinodi ya maaskofu kuhusu familia iliyohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican.

Kardinali Parolin anaendelea kuelezea kwamba, hivi karibuni, ujumbe wa Vatican umetembelea nchini China kama sehemu ya mchakato wa Vatican kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, ili kuboresha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na China, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya pande hizi mbili. Lengo ni kutaka kubomoa kuta zinazowatenganisha watu na badala yake kujenga utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya mafao ya wengi. Haya ni majadiliano kati ya Kanisa na Serikali; Kati ya Serikali na Vatican.

Majadiliano haya yanafanyika wakati ambapo Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka hamsini tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipotoa tamko kuhusu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali, Nostra Aetate. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.

Hii ni dhamana nyeti na endelevu kwa kutambua kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha binadamu na kwamba, amani inaweza kuchipua kutoka katika moyo wa mtu mwenye utulivu na amani ya kweli. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanafanya mauaji, dhuluma na nyanyaso kwa kisingizio cha dini. Viongozi wa kidini wanayo dhamana kubwa sana ya kuhakikisha kwamba, wanawasaidia waamini wao kuwa kweli ni wajenzi na watetezi wa amani.

Amani nchini Syria na huko Mashariki ya Kati ni jambo linalowezekana, ikiwa kama wanasiasa wataonesha utashi wa kisiasa pamoja na kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika kutafuta, kulinda na kudumisha amani, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 30 Novemba 2015 anatarajiwa kutembelea Barani Afrika. Kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu nchini Kenya iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ni  ”Simameni imara katika imani, msiogope”! Baba Mtakatifu anapenda kukazia upendo na huruma; umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kuponya madonda ya utengano na mpasuko wa kijamii uliojonesha nchini Kenya kwa miaka ya hivi karibuni.

Baba Mtakatifu anatembelea Uganda, ili kuadhimisha mwendelezo wa Jubilei ya miaka 50 tangu Mashahidi wa Uganda walipotangazwa na Mama Kanisa kuwa ni watakatifu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Uganda kujikita katika ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Uganda inaongozwa na kauli mbiu "Mtakuwa mashahidi wangu". Baba Mtakatifu anaendelea kufuatilia kwa masikitiko makubwa kinzani na migogoro inayoendelea kujitokeza huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati na kwamba anapenda kuonesha mshikamano wake na wote wanaoteseka.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hapo tarehe 29 Novemba 2015, anatarajia kufungua Lango la Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Bangui, Jamhiri ya Watu wa Afrika ya Kati. Anataka kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa msingi wa haki, amani na upatanisho, dhamana kwa Kanisa Barani Afrika. Kanisa linapenda kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya matumaini pasi na kukata wala kukatishwa tamaa!

Kardinali Parolin anasema, Baba Mtakatifu Francisko anasukumzwa na imani tendaji kwenda katika maeneo haya, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo, licha ya vita, kinzani na misiguano ya kijamii inayoendelea kujitokeza katika nchi hizi. Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; kwa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kuonjesha huruma kama vile Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.