2015-11-02 10:47:00

Watanzania kumbatieni Katiba mpya, ili mpate: haki, amani na mafao ya wengi!


Umoja wa wanafunzi wa Tanzania wanaoishi na kusoma mjini Roma katika maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu wote, tarehe Mosi, Novemba 2015 walikusanyika kwenye Makao makuu ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia ili kusali kwa ajili ya kuombea amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya Tanzania hasa baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika hapo tarehe 25 Oktoba 2015 kutikisa misingi ya umoja wa kitaifa, haki na amani. Viongozi wa kidini na kisiasa wanaendelea pia kuwahamasisha wananchi kuonesha ukomavu wa kisiasa na kidemorasia kwa kuambata amani na utulivu badala ya vurugu zinazoweza kulitumbukiza taifa katika maafa makubwa!

Wachunguzi wa mambo wanasema, hali bado ni tete Visiwani Zanzibar baada ya Tume ya uchaguzi ya taifa Zanzibar kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Visiwani humo. Ibada hii ya Misa Takatifu ilikuwa ni fursa ya kuwakaribisha Wakleri, Watawa na waamini walei waliotumwa na Kanisa kwa jili ya kusoma au kufanya utume hapa mjini Roma. Kwa hakika Ibada hii ya Misa Takatifu ilihudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Tanzania.

Katika mahubiri take, Padre Alcuin Nyirenda, OSB alielezea kwa ufupi yale yaliyojiri wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini Tanzania na kwamba, kwa sasa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuambata na kukumbatia Katiba mpya inayojikita katika katika haki msingi za binadamu, tayari kujenga na kudumisha amani na utulivu nchini Tanzania. Katiba mpya kadiri ya mafundisho ya Yesu inajikita katika heri nane za mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu na njia ya kuweza kuufikia utakatifu wa maisha.

Heri na nane ni dira na mwongozo wa Yesu kwa wafuasi wake na kwamba, kila mwamini anahamasishwa kugawana utajiri na rasilimali ya nchi ili wote waweze kuwa na amani, furaha na ustawi badala ya kugubikwa na ubinafsi, uchoyo na ufisadi wa mali ya umma. Watu waguswe na mahitaji ya jirani zao na wawe tayari kuwasaidia kwa hali na mali. Huzuni iwachangamotishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni vyombo na watetezi wa haki msingi za binadamu. Wapole waoneshe fadhila hii kwa kuambata upatatanisho, haki na amani badala ya kulipiza kisasi. Waamini waoneshe ile njaa ya haki, ili kweli haki ya Mungu iweze kudhihirishwa katika uhalisia wa maisha ya kijami, hapa changamoto ni kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu.

Waamini wawe ni watu wenye rehema, kwa kuhakikisha kwamba, watu wanapata mahitaji yao msingi yaani chakula, mavazi na malazi, tayari kujikita katika mchakato wa kujiletea maendeleo endelevu. Waamini wajenge utamaduni wa upatanisho, haki na amani, ili kweli waweze kuirithi nchi. Kimsingi Katiba ya Yesu itaendelea kusigana na Katiba ya walimwengu, lakini waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kuziambata na kuzimwilisha heri za mlimani, tayari kuiga utakatifu wa Mungu ili kujenga dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.