2015-11-02 11:32:00

Waamini wa Prato na Jimbo kuu la Firenze wako tayari kumpokea Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa hapo tarehe 10 Novemba 2015 kutembelea Prato na Firenze, miji iliyoko Kaskazini mwa Italia, kama sehemu ya maadhimisho ya kongamano la kumi la Kanisa Katoliki nchini Italia. Atakapowasili mjini Prato kwa Elikopta, atapata nafasi ya kutembelea Kanisa kuu la Jimbo la Prato na baadaye kuzungumza na wafanyakazi na baadaye kuondoka kuelekea Jimbo kuu la Firenze.

Akiwa Jimboni humo atatembelea Kisima cha Ubatizo na baadaye kuzungumza na wawakilishi watakaokuwa wanashiriki kwenye Kongamano la kitaifa la Kanisa Katoliki nchini Italia. Baba takatifu atawashirikisha tafakari yake na baadaye atasali sala ya Malaika wa Bwana pamoja na kuwasalimia wagonjwa watakaokuwa wamekusanyika kwenye Kanisa kuu la Kupashwa kuzaliwa kwa Bwana. Atapata chakula cha mchana na maskini na baadhi ya watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na baadaye, jioni ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.

Taarifa zinaonesha kwamba, baada ya matukio haya, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kurejea mjini Vatican kwa kutumia Elikopta, itakayotua moja kwa moja kwenye Uwanja wa ndege wa Vatican. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa na bega kwa bega ili kukujuza yale yatakayojiri wakati wa hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko, huko Prato na Firenze.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.