2015-11-02 10:11:00

Umoja na mshikamano wa kitaifa ni muhimu sana kwa mfungamano wa kijamii


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 31 Oktoba 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Gjorge Ivanon wa Yugoslavia ya Zamani pamoja na Macedonia. Baadaye Rais Ivanon alikutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Galagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Mazungumzo ya viongozi hawa wamefanyika katika hali ya amani, upendo na mshikamano kwa kuridhishwa na mahusiano ya pande hizi mbili pamoja na kupongeza jitihada zinazofanywa na Yugoslavia ya zamani katika mchakato wa ujenzi wa umoja thabiti Barani Ulaya. Wamegusia pia mahusiano ya siasa kimataifa, hususan kuhusu hali ngumu ya uchumi na kijamii pamoja na changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa msaada wa hali na mali kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi Barani Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake wameendelea kukazia umuhimu wa majadiliano na maridhiano, ili jamii iweze kuishi katika misingi ya amani na utulivu kwa kuvuka mipaka ya kidini na kijamii, tayari kuimarisha mafungamano ya kijamii na umoja wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.