2015-11-02 09:48:00

Nalikuwa mgeni mkanifariji!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaendelea kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi, changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa. “Nalikuwa mgeni, mkanifariji”, ndiyo kauli mbiu ya barua ya kichungaji kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linalowataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwaheshimu na kuwaonjesha ukarimu wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kwa sababu mbali mbali. Walinde na kudumisha uhuru na haki zao msingi, kwa kutambua kwamba, wote hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu wanahitaji msaada wao.

Kuna idadi kubwa ya Wakristo kutoka Iraq na Mashariki ya Kati wanaokimbia dhuluma na nyanyaso za kidini kutoka kwa watu wenye misimamo mikali ya kiimani. Hawa ni watu ambao maisha na utu wao vimewekwa rehani, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Waamini wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kumtenga mtu awaye yote, lakini anawaalika watu kuonesha upendo na ukarimu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawaalika viongozi wa Serikali kuonesha mshikamano kwa kutoa huduma makini kwa wahamiaji na wakimbizi pamoja na kuangalia uwezekano wa kuwaunganisha na familia zao, jambo ambalo limekaziwa na Mababa wa Sinodi ya familia, iliyohitimishwa hivi karibuni. Serikali iboreshe mazingira ili kutoa huduma bora ya makazi na afya badala ya kuwafungia kwenye kambi. Maaskofu wanaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasaidia mchakato wa haki, amani na upatanisho, ili kupunguza wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kila mtu anatekeleza wajibu na dhamana yake kwa kuonesha upendo, huruma na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji. Wanaweza kuchangia kwa hali na mali pamoja na kuyawezesha Mashiria ya misaada ya Kanisa Katoliki kuendelea kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi. Kanisa litaendelea kuboresha huduma ya kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wanasema Maaskofu Katoliki Canada.

Takwimu kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 59.5 wasiokuwa na makazi maalum kutokana na vita, kinzani za kijamii, kidini na kisiasa zinazoendelea kujionesha. Hali hii ni mbaya kuliko hata ilivyokuwa wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.