Kanisa lililopo duniani na Kanisa linaloteseka (toharani) huungana na Kanisa mshindi lililo mbinguni. Leo tunasherehekea tunayoungama kila Jumapili za mwaka - imani yetu katika ushirika wa watakatifu. Sherehe hii ilianza kusherehekewa karne ya nne (4) katika Kanisa la Mashariki kwa ajili ya kuwakumbuka mashahidi (katika ufu. Mashahidi wanaitwa watakatifu 5,8 tunasoma hivi hata alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wane na wale wazee ishirini na wane wakaanguka mbele za mwanakondoo, kila mmoja wao ana kinubi na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato ambayo ni maombi ya watakatifu) – kwanza wa Kanisa na baadaye ikawahusisha pia hata wasio mashahidi - hii ikihusisha pia Kanisa la Magharibi.
Inawahusisha wote wanaofahamika na wasiofahamika ambao wamefikia utukufu wa mbinguni. Inaamsha pia wito wetu na haja ya kuutafuta utakatifu. Inatukumbusha kwamba kwa neema ya Mungu, tunaendelea kutafuta kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na katika jina la Bwana Yesu Kristo uzima wa milele. Inatukumbusha kuwa siyo tu tunaitwa kuwa watakatifu bali sisi ni watakatifu - 2 kor. 1,1 Ef 1,1 Paulo mtume wa Kristo Yesu kwa mapokezi ya Mungu, kwa watakatifu walioko Efeso wanaomwamini Kristo Yesu, Kol 1,2 na 4,12.
NI KWANINI?
Ubatizo umetuingiza katika mwili wa Kristo. Hapo dhambi zetu zilifutwa tukawa jiwe la msingi - tukakubali kujengwa juu yetu nyumba ya kiroho, ukuhani mtakatifu na kutoa sadaka hai zinazompendeza Mungu - 1Pt 2.5. Katika harakati zetu za kusaka utakatifu tunategemea maongozi ya Roho Mtakatifu kutuongoza, kutufundisha na kutukumbusha yote aliyosema Bwana - Yoh 14,26. Roho Mtakatifu anatufundisha kusali, anatusaidia katika unyonge wetu – Rum 8:26-27. Katika kipaimara tumeunganisha na kukomazwa katika neema ya ubatizo katika kuweza kumuita Mungu ABA - Rum. 8, 15, kutuimarisha katika Kristo, kuongeza mapaji ya Roho Mtakatifu ndani yetu, kutakatifuza mahusiano yetu na kanisa - LG 11, hutupatia neema ya pekee ya kueneza na kulinda imani yetu kwa maneno na matendo katika kumshuhudia Kristo, kuliungama jina la Bwana na kuulinda msalaba - Mtaguso wa Florence 1439,DS 1319,LG 11, CCC1309.
Katika masomo yetu
Mtakatifu Theresia wa mtoto Yesu alizoea kusema anaishi mbingu akitenda mema hapa duniani. Katika macho yetu hatumwoni sasa, lakini tunashiriki matunda ya maisha yake anayoyaishi sasa kiukamilifu huko mbinguni. Tunapaswa kujua kwamba kufika mbinguni siyo jambo rahisi pia, ingawa inawezekana kabisa ila hatuna budi kutoka jasho. Neno hili la Mungu litupe changamoto - Mt. 6,21 tunasoma hivi kwa kuwa hazina yako ilipo ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Na pia katika Mt. 7,21 tunasoma hivi si kila mtu aniambiaye Bwana, Bwana atakayeingia katika ufalme wa mbinguni bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
Ni namna gani basi tuishi na kutimiza mapenzi ya Baba wa mbinguni hapa duniani ili tuweze kuzirithi mbingu? Tazama Injili ya leo Mt. 5:1-12 heri nane. Hapa Yesu anatupatia ramani ya matembezi yetu hapa duniani katika kuuendea uzima wa milele. Hawa tunaowasherehekea leo walipitia njia hii ya heri. Leo nasi tunaitwa na kupewa tena changamto na kukumbushwa kuifuata hiyo ramani. Hizi heri zatuonesha njia ya mbinguni. Twaitwa tuwatambue na tujitambue na wale walio maskini wa hali na mali, wanaolia, wapole, wenye njaa, wenye kiu ya haki n.k. zatumihiza tuwahurumie wengine, tuwe safi rohoni na kuwa watu wa amani kati ya mtu na mtu, na familia zetu katika jamii hata kama kufanya hivyo hakutupatii faida yoyote kwa sasa. Huku ndiko kuwekeza mbinguni. Watakatifu wetu hawa walifanya kadiri ya mapenzi yake Mungu. Sote twajua huwezi kupata bila kutoa, bila kuwekeza. Mtaka cha uvunguni sharti ainame.
Mfano: bibi mmoja aliyekuwa tajiri hapa duniani. Alipofariki akapata bahati ya kufika mbinguni. Malaika akampokea na akaanza kumwongoza kumpeleka mahali ambapo aliandaliwa kukaa. Akawa anakatiza mitaa ya mbinguni na kuona fahari zake na uzuri wake. Walipofika mahali alipopangiwa kukaa, akaona vitu vichache visivyo na uzuri na thamani ya pekee. Akamwambia yule Malaika, mbona unaniweka hapa na vitu vilivyopo si vingi na vizuri kama walivyonavyo wenzangu? Malaika akamwambia, bibi mpendwa ridhika na ulichopata. Vifaa vya ujenzi ulivyotuma toka duniani vilitosha tu kuandaa kibanda hiki. Malaika akamwacha akaenda zake. Nasi Je, ni kitu gani tunawekeza mbinguni?
Pengine watakatifu ni wale wakubwa yaani Mitume na Manabii - Efe. 3,5; Kol 1,26 - mwishoni katika AK, Ayubu, malaika wanaitwa watakatifu Mk 8,38; Lk 9,26, Uf, 14,10 pengine ni vigumu kujua kama aya fulani zinasema juu ya malaika au watu walio katika utukufu wa mbinguni - Efe 1,18,Kol 1,12 1 Thes 3,13. Katika Rum 1,7 tunasoma hivi kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu walioitwa kuwa watakatifu neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Katika 1 Kor 1,2 tunasoma pia kwa Kanisa la Mungu lililoko Korintho wale waliotakaswa katika Kristo Yesu walioitwa wawe watakatifu pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali Bwana wao na wetu. Mtakatifu Paulo asema kazi ya watakatifu ni kuwahudumia watakatifu wengine Rum 12,13; 15:15-16, 1 Kor 16,1, 2 Kor, 8,4; 9,1 ebr 6,10 maana Mungu si dhalimu hata aisahau kazi yenu ya pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Yeye aliishi hivyo angalia maandiko yake.
Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©. |