2015-10-31 08:47:00

Wafiadini wa Kanisa ni hazina ya imani, matumaini na mapendo kati ya watu!


Mashuhuda wa imani ni amana na urithi mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni watu ambao wameteseka, wakadharauliwa na kunyanyasika, lakini hatimaye, Mwenyezi Mungu amewaonesha utukufu wake kama ilivyokuwa kwa Mwenyeheri Oscar Arnulfo Romero. Alikuwa mchungaji mwema, aliyejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa; akaonesha upendo mkuu kwa Mwenyezi Mungu na jirani zake, kiasi hata cha kufa shahidi wa Kristo na Kanisa lake.

Kwa ufupi, huu ndio ujumbe uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 30 Oktoba 2015 alipokutana na umati wa mahujaji kutoka Salvador, waliofika mjini Vatican kumshukuru Baba Mtakatifu kwa kumtangaza Askofu mkuu Romero kuwa Shahidi. Ni kiongozi wa Kanisa aliyejitahidi kumwilisha heri za mlimani katika maisha na utume wake, akawa kweli ni chemchemi ya furaha kwa wote aliokutana nao.

Mwenyeheri Romero alimpenda Mungu upeo, kiasi cha kuyamimina maisha yake wakati akiwa anaadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu unaojidhihirisha kwa njia ya Fumbo la Msalaba, chemchemi ya Injili inayotangazwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Kwa hakika kama wanavyosema Mababa wa Kanisa, damu ya mashuhuda wa imani ni mbegu ya Ukristo, itakayozaa matunda ya utakatifu wa maisha, haki, upatanisho na upendo kwa wakati wake.

Askofu mkuu Romero alipenda kuwahamasisha waamini kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Mashuhuda wa imani ni wenzi katika hija ya maisha ya kiroho katika kweli na utakatifu, licha ya magumu na mateso ambayo waamini wanaweza kukabiliana nayo katika maisha. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Padre Rutilio Grande aliyejisadaka kwa ajili ya Injili ya Kristo. Mashuhuda hawa wa imani ni hazina na msingi wa Kanisa na jamii ya watu wa  El Salvador.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, iwe ni fursa ya kupyaisha mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili, ili huruma na upendo wa Mungu uweze kuwafikia na kuwagusa watu wengi zaidi nchini El Salvador, kama ilivyokuwa kwa njia ya ushuhuda wa Askofu mkuu Romero. Familia ya Mungu nchini Salvador bado inakumbana na changamoto nyingi katika maisha yake, changamoto kwa Kanisa zima kuwa ni mihimili ya Uinjilishaji inayoshuhudia katika umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa.

Anasema, Kanisa linapaswa kujipambanua kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu wenye kiu ya haki, amani na upatanisho unaojikita katika mioyo ya watu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia wananchi wote wa  El Salvador, imani, matumaini na mapendo; ili wote waweze kujisikia kuwa kweli ni ndugu wamoja katika Kristo Yesu. Kifodini cha Askofu mkuu Romero ulikuwa ni mchakato wa muda mrefu uliojikita katika ushuhuda, katika mateso, dhuluma na nyanyaso. Hata baada ya kifo chake, alizushiwa mengi, akapakwa matope na kuchafuliwa jina na heshima yake hata na ndugu zake katika Ukuhani, lakini bado akaendelea kuwa ni shuhuda wa Injili ya Kristo. Ni Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anayefahamu fika historia ya maisha ya mja wake, hata kama mashuhuda hawa wa imani wanaendelea kuteswa kwa njia ya upanga wa ulimi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.