2015-10-31 15:24:00

Wafanyabiashara Wakristo onesheni ushuhuda wenye mashiko kwa kuzingatia maadili


Umoja wa Wafanyabiashara wa Kikristo nchini Italia, UCID, unapania pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, waamini hawa wanakuwa kweli ni vyombo na chachu ya maendeleo kwa ajili ya mafao ya wengi. Ili kufikia lengo hili, wajumbe wa umoja huu hawana budi kufundwa barabara ili waweze kuelewa mafundisho Jamii ya Kanisa, tayari kuyamwilisha katika sera na mikakati ya maendeleo katika maeneo yao. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaishi kiaminifu kwa kujikita katika weledi wao ili kutekeleza malengo ya umoja huu katika mazingira wanamoishi.

Wanachama wawe tayari kujiendeleza, ili kuwa kweli ni chachu ya mageuzi na maendeleo kwa njia ya maneno, lakini zaidi ushuhuda wa maisha yao katika ulimwengu wa wafanyabiashara unaokabiliwa na changamoto nyingi! Kwa vile umoja huu unatambuliwa na Kanisa, kumbe wanachama wake wanapaswa kuwa waaminifu kwa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa katika familia, maeneo ya kazi na ndani ya jamii katika ujumla wake. Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Kikristo nchini Italia, Jumamosi, tarehe 31 Oktoba 2015. Huu ni mwaliko wa kumwilisha ari na mwamko wa kimissionari kama waamini walei, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, rasimali ya dunia inatumiwa vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wote.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wafanyabiashara kutumia maeneo yao ya biashara kama vituo vya kujipatia utakatifu wa maisha; mahali pa kujenga na kuimarisha umoja, udugu na mshikamano kati ya wafanyabiashara, viongozi na wafanyakazi wao, kwa kuwajibika pamoja na kutafuta mafao ya wengi. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira mazuri, kwa kutambua kwamba, rasilimali watu ni muhimu sana katika mchakato wa uzalishaji unaopaswa kuzingatia uwiano mzuri kati ya kazi na familia.

Haki msingi za wafanyakazi kama vile: muda wa kazi, likizo ya uzazi na mapumziko, zitambuliwe na kuheshimiwa. Wafanyabiashara pia wanahamasishwa na Mama Kanisa kulinda na kutunza mazingira, nyumba ya wote, ili maendeleo ya kweli yanayomgusa binadamu kwa kujikita katika mafungamano thabiti ya kijamii. Baba Mtakatifu anasema, huu ni mwelekeo wa Injili katika masuala ya kijamii ambayo kimsingi yana changamoto nyingi. Wawe makini kuguswa na umaskini na hali ngumu ya wafanyakazi, ili kujenga na kudumisha mshikamano na wananchi kutoka sehemu mbali mbali za Italia, kielelezo makini cha umwilishaji wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, shughuli zote za uzalishaji kiuchumi hazina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya binadamu na mafao ya wengi. Huu ndio mwelekeo wa Kiinjili katika masuala ya kiuchumi; kwa kushikamana katika shughuli za uzalishaji na huduma kwa kuongozwa na kanuni auni na maadili, ili kukabiliana na changamoto pamoja na vishawishi vinavyoweza kujitokeza katika masuala ya biashara. Wanachama wawe na ujasiri wa kufanya tafiti ili kuangalia mchango wao katika shughuli za uzalishaji na huduma, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahamasisha wafanyabiashara, Serikali, wachumi na wadau mbali mbali kujikita katika misingi ya maadili, ukweli, uwazi na uaminifu pamoja na uwajibikaji makini. Kanuni maadili itoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na jumuiya yake na matunda ya mikakati hii yataweza kupimwa mintarafu mwanga wa Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.