2015-10-31 09:23:00

Shikamaneni kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto ya wahamiaji Barani Ulaya


Viongozi wa Makanisa Barani Ulaya, katika tamko lao lililotolewa hivi karibuni wanawataka viongozi wa Serikali na Kisiasa kuwa na mwelekeo wenye uwiano bora wakati huu wanapoendelea kukabiliana na changamoto ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya. Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, ametembelea kambi nyingi za wakimbizi na wahamiaji na kushuhudia mateso na mahangaiko ya watu hawa.

Mashirika ya Misaada ya Makanisa yako mstari wa mbele katika kuwahudumia wakimbizi kwa hali na mali, changamoto na mwaliko kwa viongozi wa Kiserikali na Kisiasa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza vyema dhamana na wajibu wao; kwa kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya binadamu. Changamoto ya wakimbizi inapaswa kushughulikiwa kwa kujikita katika mshikamano, ushirikiano na urafiki ili kuweza kuipatia changamoto hii ufumbuzi wa kudumu.

Huu pia utakuwa ni mwanzo mzuri wa kukabiliana na matatizo mengine yanayojitokeza katika huduma kwa wahamiaji na wakimbizi. Makanisa yataendelea kuchangia katika sera na mikakati ya huduma za kichungaji na maisha ya kiroho kwa wahamiaji na wakimbizi; kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu kama anavyo kaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Jumuiya ya Ulaya inayo dhamana ya kimaadili kuhakikisha kwamba, inawapokea na kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi wanaoendelea kumiminika Barani Ulaya kutoka katika maeneo yenye vita, kinzani na migogoro ya kijamii.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015, kumekuwepo na wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya. Serikali na Makanisa washirikiane ili kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi; kwa kuheshimu haki msingi za binadamu pamoja na kuhakikisha kwamba, vita huko Syria na Mashariki ya Kati inapata ufumbuzi wa kudumu. Makanisa yaendeleze majadiliano ya kiekumene, ili kuweza kupata majibu msingi katika kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaotoka kwenye dhiki wanapaswa kuhudumiwa na kusaidiwa na kwamwe si kutelekezwa na kunyanyaswa, kwani licha ya matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo, wao pia wanabeba utajiri mkubwa katika maisha yao. Wakimbizi na wahamiaji si mzigo bali ni rasilimali kubwa inayoweza kusaidia katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.